tuwasiliane

Saturday, January 14, 2017

Cheche: "Mimi ni Kocha Mkubwa na Mwenye Bahati"

Iddi Cheche kocha Azam FC
Aliyekuwa kocha mkuu wa kikosi cha mabingwa wa Kombe la Mapinduzi 2017 Azam FCNassor Iddy 'Cheche' amesema kubeba taji hilo kumemfanya ajione kocha mkubwa na mwenye bahati kwasababu amezifunga timu kubwa zinazofundishwa na makocha kutoka nje ya Tanzania.

Cheche amekiambia chanzo kimoja,  michuano  hiyo imempa heshima kubwa na kurudisha hadhi ya timu yake  ambayo ilipotea tangu kuanza kwa msimu huu kwenye ligi ya Vodacom hata mwanzoni mwa michuano hiyo.

"Najipongeza Mimi mwenyewe kwa kuweza kuumudu mtihani niliopewa na uongozi wa kuileta timu kwenye michuano ikiwa imebaki wiki moja huku mwenendo wake kwenye ligi ukiwa siyo mzuri ukweli nimetumia vizuri taaluma yangu na kujijengea heshima kubwa mbele ya makocha wa Simba na Yanga timu ambazo nimezifunga"

"Lakini pia nawapongeza wenzangu wa benchi la ufundi na wachezaji ambao walicheza kwa kujitoa na hadi kufika fainali n.a. kuwa mabingwa kwa mara ya tatu kwenye michuano hii ukweli kazi haikuwa rahisi ilibidi tupambane maana tuliamka vibaya na hatukuwa  tukipewa nafasi ya ubingwa," amesema Cheche.

Kocha huyo wa muda amesema anarudi Dar es Salaam, akijivunia mafanikio hayo na yupo tayari kurudi kwenye timu yake ya vijana U-20, ambayo ndiyo anayoifundisha kabla uongozi kumpandisha timu ya wakubwa baada ya kutimuliwa kwa Mhispania Zeben Hernandez.

Amesema kazi aliyotumwa amesha imaliza hivyo kama mwajiriwa atausikiliza uongozi kama utapenda abaki kwenye kikosi cha timu hiyo kama msaidizi wa kocha mpya  Mromania ambaye atakabidhiwa kwa timu hiyo kesho jumapili baada ya timu kurudi Dar es Salaam.
Azam iliyokuwa chini ya kocha Cheche, ilifanya maajabu ya mwaka kwa kuifunga Yanga mabao 4-0 , katika mchezo wa hatua ya makundi kabla ya jana usiku kuifunga Simba bao 1-0,  katika mchezo wa fainali uliopigwa uwanja wa Amaan Zanzibar.

No comments:

Post a Comment