tuwasiliane

Saturday, January 14, 2017

Azam FC yatwaa Mapinduzi Cup, yaweka rekodi ya hatari

NI raha tu! Hivi ndivyo hali ilivyo kwa timu ya Azam baada ya usiku wa kuamkia leo kutwaa taji la michuano ya Kombe la Mapinduzi, ikiichapa Simba bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Klabu hiyo Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, imetwaa taji hilo kwa kuandika rekodi mpya na ya aina yake baada ya kutofungwa mchezo wowote katika mechi tano ilizocheza za michuano hiyo, huku pia ikiwa haijaruhusu bao lolote.
Azam FC ikicheza kwa ari kubwa na morali ya hali ya juu kwenye mchezo huo, iliwachukua dakika 13 tu kuweza kuandika bao hilo la ushindi lililofungwa kiufundi kwa shuti kali la umbali wa mita 25 na Nahodha Msaidizi, Himid Mao ‘Ninja’.
Mao alipiga shuti hilo lililomshinda kipa wa Simba, Daniel Agyei, kufuatia pasi safi aliyopigiwa na kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’.
Licha ya Simba kufanya mashambulizi kadhaa, ilijikuta ikutana na upinzani mkali wa kuweza kuipenya safu ngumu ya ulinzi ya Azam FC chini ya mabeki wa kati visiki, Aggrey Morris na Yakubu Mohammed.
Haikushangaza kusikia mwishoni mwa mchezo huo, Morris akitangazwa kuwa mchezaji bora wa mechi hiyo na kupewa zawadi ya katoni nne ya kinywaji safi cha Azam Malti, kiatu cha kuchezea mpira na kikombe maalum.
Azam FC kutwaa ubingwa huo, kumeifanya kujibebea kombe walilokabidhiwa na mgeni wa heshima wa mchezo huo Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, pia walijizolea medali na kitita cha Sh. Milioni 10 na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, huku Simba wakipewa medali za mshindi wa pili na Sh. Milioni 5.
Kamati ya mashindano hayo pia ilimtangaza kipa wa Azam FC, Aishi Manula, kuwa Kipa Bora wa michuano hiyo, Beki Bora amekuwa ni Mzimbabwe Method Mwanjali wa Simba na Mfungaji Bora ni Simon Msuva wa Yanga.
Taji la tatu
Ubingwa huo umeifanya Azam FC kuifikia rekodi ya Simba ya kulitwaa taji hilo mara tatu, lakini mabingwa hao safari hii wakibebwa na rekodi ya kulitwaa bila kufungwa mchezo wowote wala kuruhusu wavu wake kuguswa.
Mara mbili za nyuma, iliweza kuweka rekodi ya kuwa timu pekee kulitwaa taji hilo mara mbili mfululizo, ikilibeba mwaka 2012 na 2013.
Rekodi zakolea Azam FC   
Ubingwa huo unaifanya Azam FC kufikisha taji la pili msimu huu na hii ni baada ya Agosti mwaka jana kutangulia kwa kutwaa Ngao ya Jamii kwa kuifunga Yanga kwa mikwaju ya penalti 4-1 kufuatia sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90.
Hiyo ni rekodi ya pili mfululizo kwa Azam FC kutwaa taji bila kuruhusu wavu wake kuguswa, itakumbukwa walifanya tena hivyo mwaka juzi walipotwaa taji la kwanza la michuano ya Kombe la Kagame (CECAFA Kagame Cup), ambapo kwenye fainali waliichapa Gor Mahia mabao 2-0.
Msimu wa 2013/2014, Azam FC ilifanya maajabu mengine ya kutwaa taji la kwanza la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) bila kufungwa mchezo wowote.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa:
Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gadiel Michael, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Stephan Kingue, Salum Abubakar, Himid Mao/Enock Atta Agyei dk 82, John Bocco, Yahya Mohammed/Mudathir Yahya dk 69, Joseph Mahundi/Frank Domayo dk 57

No comments:

Post a Comment