tuwasiliane

Saturday, January 14, 2017

Afcon 2017: Michuano ya mataifa Afrika kuanza

Issoze Ngondet
Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika, makala ya 31, itang'oa nanga Jumamosi saa 16:00 GMT (saa moja jioni Afrika Mashariki) pale wenyeji watakapokabiliana na Guinea-Bissau ambao wanashiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza.
Miaka sitini imepita tangu kuchezwa kwa fainali za kwanza za kuamua Taifa Bingwa Afrika, ambayo ilichezewa nchini Sudan mwaka 1957.
Ni mataifa matatu pekee yaliyoshiriki na mshindi alikuwa Misri.
Mwaka huu kutachezwa mechi 32 katika kipindi cha siku 23 na kushirikisha timu 16.
Michuano itaanza kwa hatua ya makundi, ambayo ni manne kila moja likiwa na mataifa manne.
Mshindi atajulikana kwenye fainali tarehe 5 Februari na kupokezwa kikombe kilichoundiwa Italia pamoja na zawadi ya $4m.
Waafrika wanaendelea kuchangamkia michuano hiyo, ambayo bila shaka imeibuka kuwa kubwa zaidi ya soka barani Afrika.
Wenyeji Gabon wanaandaa michuano hiyo kwa mara nyingine miaka mitano tu baada ya kuwa mwenyeji kwa pamoja na Equatorial Guinea.
Walipewa fursa ya kuwa wenyeji baada ya kujiondoa kwa Libya kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Gabon ndilo taifa lililoorodheshwa chini zaidi orodha ya viwango vya soka ya FIFA mwezi Januari miongoni mwa timu zinazoshiriki, ambapo iliorodheshwa nambari 108.
Hata hivyo wana mchezaji nyota, Pierre-Emerick Aubamenyang anayechezea Borussia Dortmund ya Ujerumani.Kando na Aubameyang, wengi watakuwa pia wanamtazama sana Mchezaji Bora wa Mwaka Afrika wa BBC na CAF Riyad Mahrez wa Algeria pamoja na mchezaji ghali zaidi Afrika Sadio Mane.Kutoka Ligi ya Premia, kutakuwa na nyota wa Manchester United Eric Bailly kutoka Ivory Coast, Andre Ayew wa West Ham na Ghana, Islam Slimani wa Leicester City na Algeria na nyota wa Crystal Palace kutoka Ivory Coast Wilfried Zaha.
Raia wa Misri Mohamed Salah ameng'aa sana tangu alipohama Chelsea na kujiunga na Roma ya Italia.
Ni mara ya kwanza kwa Uganda kucheza michuano hiyo baada ya miaka 39 na wana kipa Denis Onyango aliyeshinda tuzo CAF ya mchezaji bora Afrika anayecheza ligi za ndani ya bara.

No comments:

Post a Comment