tuwasiliane

Friday, December 30, 2016

Ronaldo akataa mshahara wa £1.6m kwa wiki kutoka klabu ya China

Ronaldo na mkufunzi wa Real Madrid Zinedine Zidane
Klabu ya Real Madrid ilipewa takriban pauni milioni 250 na klabu ya China ambayo haikutajwa jina ili kumnunua nyota wake Cristiano Ronaldo kulingana na ajenti wake Jorge Mendes.
Amesema kuwa nahodha huyo wa Portugal mwenye umri wa miaka 31 hana haja na mpango huo ambao ulishirikisha mshahara wa kila mwaka wa pauni milioni 85.
Ronaldo alisema kuwa anaweza kucheza kwa miaka mingine 10 mnamo mwezi Novemba baada ya kuandikisha mkataba mpya na Real Madrid hadi Juni 2021.
''Soko la China ni soko jipya.wanaweza kuwanunua wachezaji wengi, lakini haiwezekani kumnunua Ronaldo'', alisema Mendes.
''Cristiano ndio mchezaji bora duniani, ni kawaida kupata maombi'', aliongezea raia huyo wa Ureno.
Chini ya ombi hilo analodai Mendes, Ronaldo angepokea kitita cha pauni milioni 1.6 kwa wiki ikiwa ni mara tatu ya zaidi ya kitita cha uhamisho wa pauni milioni 89 zilizogharimu uhamisho wa Paul Pogba kutoka Juventus kuelekea Manchester United.
Mendes aliambia Sky Italia: Klabu ya China imetoa pauni milioni 257 kwa Real Madrid na zaidi ya Yuro milioni 100 kila mwaka kwa Ronaldo.
''Lakini fedha sio kila kitu.Klabu hiyo ya Uhispania ndio maisha yake''.
Hatua hiyo inajiri baada ya klabu ya Shanghai Shenhua kutoka China kuthibitisha kwamba imemsajili aliyekuwa mshambuliaji wa Manchester City Carlos Tevez kutoka klabu ya Boca Juniors.
Shanghai inayofunzwa na aliyekuwa mkufunzi wa Brighton Gus Poyet ,wameripotiwa kukubali uhamisho wa pauni milioni 40 mbali na mshahara wa zaidi ya pauni milioni 310,000 kwa wiki.

No comments:

Post a Comment