tuwasiliane

Friday, December 2, 2016

KOCHA MPYA MSAIDIZI MZAMBIA AWASILI YANGA, KUSAINI LEO


WAKATI kiungo Justine Zullu Jana alisaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na Yanga SC, Kocha Mkuu mpya, George Lwandamina ameanza kulifanyia marekebisho na benchi la Ufundi la klabu hiyo, baada ya kumleta Msaidizi wake maalum, Mzambia mwenzake, Noel Mwandila.
Kiungo wa zamani wa Green Buffaloes ya Zambia, Noel Mwandila aliwasili Dar es Salaam juzi na jana kutwa nzima alikuwa na mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo na leo anatarajiwa kusaini mkataba. 
Mwandila aliwasili siku moja baada ya kiungo Mzambia, Justine Zullu kuwasili pia nchini kwa mazungumzo ya kujiunga na mabingwa hao wa Tanzania.Na kama Mwandila pia akijiunga na Yanga, maana yake klabu hiyo itakuwa na Wazambia wanne pamoja na Zullu, baada ya kocha Lwandamina na kiungo Obrey Chirwa.

Mwandila atapanua benchi la Ufundi la Yanga akiungana na wazalendo Juma Mwambusi ambaye ni Kocha Msaidizi, Juma Pondamali kocha wa makipa chini ya Mkurugenzi wa Ufundi, Mholanzi Hans van der Pluijm.
Maofisa wengine katika benchi la Ufundi la Yanga ni Meneja Hafidh Saleh, Daktari Edward Bavu, Mtunza Vifaa Mohammed Omar ‘Mpogolo’ na Mchua Misuli, Jacob Onyango.
Yanga jana iliendelea na mazoezi kwa siku ya pili kwenye Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Na idadi ya wachezaji imeongezeka hadi kufika 23 tangu mabingwa hao wa Tanzania Bara waanze mazoezi Jumatatu na maanaa yake sasa wanakosekana wachezaji wawili tu, ambao ni beki Mtogo, Vincent Bossou ambaye ana ruhusa maalum na kiungo chipukizi, Yussuf Mhilu aliyepandishwa msimu huu kutoka timu ya vijana, yupo na kikosi cha U-20 Bukoba mkoani Kagera kwenye Ligi Kuu ya Vijana.Waliofika hadi sasa ni makipa Ally Mustafa ‘Barthez’, Deo Munishi ‘Dida’, Benno Kakolanya, mabeki Hassan Kessy, Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Kevin Yondan, Pato Ngonyani, Juma Abdul, Andrew Vincent ‘Dante’ na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Wengine ni viungo Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Mkongo Mbuyu Twite, Geofrey Mwashiuya, Juma Mahadhi, Said Juma, Mzimbabwe Thabani Kamusoko na washambuliaji Mrundi Amissi Tambwe, Mzimbabwe Donalde Ngoma, Malimi Busungu na Matheo Anthony.
Na Yanga inajiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika mapema mwakani.
Wakati huo huo: Kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Justine Zullu jana amesaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na Yanga SC.
Hata hivyo, haijulikani mchezaji gani wa kigeni ataachwa ili timu ibaki na wachezaji saba kwa mujibu wa kanuni wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Wachezaji wengine wa kigeni wa Yanga ni mabeki Mbuyu Twite kutoka DRC, Vincent Bossou kutoka Togo, viungo Haruna Niyonzima wa Rwanda, Thabani Kamusoko wa Zimbabwe na washambuliaji Mrundi Amissi Tambwe, Mzimbabwe Donalde Ngoma na Mzambia, Obrey Chirwa.

No comments:

Post a Comment