tuwasiliane

Friday, December 2, 2016

HATIMAYE FARID APATA KIBALI CHA KAZI HISPANIA



KIUNGO chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Farid Mussa Malik sasa anaweza kwenda Hispania kujiunga na klabu yake, CD Tenerrife ya Daraja la Kwanza, maarufu kama Segunda B.
Hiyo inafuatia kupatiwa kibali cha kuishi na kufanya kazi nchini Hispania ambacho kinatarajiwa kuwasili leo nchini.
Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online , Farid ambaye hajacheza mechi yoyote msimu huu kwa kuchelewa kupata kibali, alisema kwamba Tenerife ndiyo wamemtumia taarifa juu ya kibali chake.
“Tenerife wamenitumia taarifa kwamba kibali kimepatikana na wamempa mtu anakuja nacho kuja kunikabidhi mkononi ili niende Hispania kuanza kazi,”alisema.



Farid alisema anakisubiri kwa hamu kibalo hicho, kwa kuwa amekaa muda mrefu bila kucheza na sasa ana anataka kurudi uwanjani.    
Azam FC imemtoa kwa mkopo Farid kwenda CD Tenerife kwa makubaliano maalum. Na hiyo ilifuatia Farid kufuzu majaribio katika klabu hiyo katikati ya mwaka alipokwenda na Mkurugenzi wa klabu yake, Yussuf Bakhresa.
Farid alitua Hispania Aprili 21 baada ya kuichezea Azam FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance mjini Tunis, Tunisia ikifungwa 3-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya awali kushinda 2-1 Dar es Salaam.
Na ilimchukuwa wiki moja tu Farid kuwakuna kwa kipaji chake makocha wa Tenerife na kutaka kumnunua, lakini Azam ikakataa na kuamua kumtoa kwa mkopo.
Azam FC haijamsajili Farid katika kikosi chake cha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu kwa kuwa imemtoa kwa mkopo Tenerife ambayo tayari imemuombea hadi Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC). 

No comments:

Post a Comment