tuwasiliane

Wednesday, December 7, 2016

Bossou amkubali Lwandamina

Vincent Bossou | Yanga
MlinziI wa kati wa Yanga  raia wa Togo Vicent Bossou, amemwagia sifa kocha mpya wa timu yake Mzambia George Lwandamina, kwa kusema mazoezi yake ni kielelezo tosha cha wao kwenda kutetea ubingwa wao msimu huu.
Bossou ameiambia Goal, mazoezi ya Lwandamina,  yamekuwa na utofauti mkubwa na mtangulizi wake Mdachi Hans van der Pluijm, ambaye ndiye aliyemsajili kwenye kikosi hicho akitokea kwao Togo mwanzoni mwa msimu uliopita.
“Nashukuru nimeanza vizuri ingawa mazoezi yamekuwa magumu,  siku ya kwanza lakini mambo siyo mabaya huu ni mwanzo mzuri chini ya kocha Lwandamina ambaye naamini atatufikisha mbali kutokana na mbinu na ufundishaji wake,”amesema Bossou.

Beki huyo amesema anafurahi kuona hamasa ya wachezaji imeongezeka ndani ya timu na kila mmoja anafanya mazoezi kwa bidii, kitu ambacho kinampa matumaini ya kuweza kutetea ubingwa wao wakiwa chini ya kocha huyo mpya.
Amesema anatambua ushindani utakao kuwepo kati yao na vinara wa ligi Simba, lakini kasi waliyokuwa nayo hivisasa itawawezesha kuwapindua wapinzani wao Simba na wao kukaa kileleni kwa mara ya kwanza msimu huu.
“Tumebakiza pointi mbili dhidi ya Simba, ili tuongeze ligi, nijambo gumu lakini linawezekana kutokana na kasi tuliyokuwa nayo hivi sasa kila mchezaji anataka kucheza kwa bidii ili kutafuta nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza,”amesema Bossou.
Mchezaji huyo amesema amerudi kwenye kikosi hicho na mipango yake ni kuhakikisha anarudi kwenye kikosi cha kwanza kama ilivyokuwa kwa kocha  Van der Pluijm, ambaye alimtumia kama mchezaji wa kikosi cha kwanza baada ya kuridhishwa na kiwango chake.
Mchezaji huyo anamaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu, na kunauwezekano akabaki kuichezea timu hiyo, kama kocha Lwandamina ataridhishwa na kiwango chake  kwenye mzunguko wa pili wa ligi hiyo iliyopangwa kuanza Desemba 17.

No comments:

Post a Comment