tuwasiliane

Wednesday, December 21, 2016

Azam FC kuanzia raundi ya kwanza CAF

img_0037
SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limepanga droo ya Kombe la Shirikisho Afrika (CC), inayoonyesha kuwa Azam FC inaanza kufungua dimba la michuano hiyo kwa kucheza raundi ya kwanza.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Azam FC kupangwa kuanzia raundi hiyo inayohusisha timu zenye ubora tofauti na zile zinazoanzia raundi ya awali (preliminary round).
Droo hiyo inaonyesha kuwa, Azam FC itacheza na mshindi wa jumla wa mechi ya raundi ya awali kati ya Orapa United ya Botswana na Mbabane Swallows ya Swaziland.
Azam FC itaanzia kucheza ugenini na moja kati ya timu hizo itakayoibuka kidedea kati ya Machi 10 hadi 12 mwakani kabla ya kurejeana nyumbani Azam Complex kati ya Machi 17 na 19.
Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii wakifuzu hapo, wataingia raundi ya mwisho ya mtoano (play off), ambapo itakutana na moja ya timu 16 zilizotolewa kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikipenya tena hapo itaingia moja kwa moja kwenye hatua ya makundi.
Hatua hiyo ya makundi itakayoanza Mei mwakani, itahusisha timu 16 zilizogawanywa kwenye makundi manne, zitakazocheza mechi sita (tatu nyumbani na tatu ugenini), washindi wawili wa kila kundi wataingia robo fainali.

No comments:

Post a Comment