tuwasiliane

Wednesday, November 30, 2016

YANGA KUMPA TAMBWE MKATABA MPYA SOON

HD Amissi Tambwe
Mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga Amissi Tambwe yupo mbioni kusaini mkataba mpya, baada ya uongozi wa timu hiyo kuridhishwa na kiwango chake.
Katibu Mkuu wa Yanga Baraka Deusidedit, amekiambia chanzo chetu kuwa, wametathimini kiwango cha mchezaji huyo na kugundua bado anahitajika ndani ya timu yao na sasa wanamuandalia mkataba mpya ili atakaporudi kutoka mapumziko aweze kusaini.

“Kamauongozi kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Ufundi Hans van der Pluijm, tumekitathmini kiwango chake na kukubaliana tumuongezee mkataba wa miaka miwili kwasababu bado timu inahitaji mchango wake,”amesema Baraka.
Kiongozi huyo amesema pamoja na umri mkubwa aliyokuwa nao nyota huyo kutoka Burundi, lakini wanaridhishwa na kile anachokifanya kwenye timu yao na ndiyo maana wamekuwa wakimuongezea muda kila ule wa awali unapomalizika.

Amesema pamoja na msimu huu kuonyesha kiwango cha chini lakini bado wanaimani naye na kuamini ataweza kutetea tuzo yake ya mfungaji bora aliyoipata msimu uliopita kwa kufunga mabao 21 katika ligi ya Vodacom.

“Ukweli pamoja na watu kusema kwamba amechoka hana tena uwezo lakini sisi hilo hatuliangalii kwasababu rekodi yake ya ufungaji bado nzuri ukiangalia msimu huu anashika nafasi ya pili akiwa na mabao saba amepitwa mabao mawili na Shizza Kichuya anayeongoza ,”amesema Baraka.
Kiongozi huyo amesema kwa rekodi aliyokuwa nayo Tambwe kwenye ligi ya Tanzania amesema ni vigumu kumuachia mshambuliaji huyo aondoke kwani bado wanahitaji mchango wake ukizingatia ugumu wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wanayokwenda kushiriki mapema mwakani.
Tambwe amebakiza miezi sita ili mkataba wake kumalizika na hivi karibuni kulienea uvumi kwamba mshambuliaji huyo ni miongoni mwa nyota wawili wa kimataifa watakaotemwa na kocha George Lwansamina ili kutoa nafasi ya kusajiliwa kwa wachezaji wengine wawili ambao ni Jesse Were mshambuliaji na Meshacky Chaila.

No comments:

Post a Comment