tuwasiliane

Sunday, November 6, 2016

Ni Mbao v Azam FC CCM Kirumba leo


BAADA ya kuzoa pointi zote tisa ndani ya mechi tatu zilizopita za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), Azam FC itakuwa na kibarua kingine leo Jumapili pale itakapowavaa wenyeji wao Mbao FC ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza saa 10.00 jioni.
Kikosi cha Azam FC kipo fiti na imara zaidi baada ya kutoka kuzifunga JKT Ruvu (1-0), Kagera Sugar (3-2) na Toto African (1-0), mechi ambazo zimeongeza morali ya hali ya juu kwenye kikosi hicho baada ya kutoanza vema ligi hiyo.
Tena ikiifunga Toto African na kuandika rekodi mpya kwa kuifunga kwa mara ya kwanza ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba tokea Septemba 24, 2008 ilipocheza nayo kwa mara ya kwanza.
Hii ni mara ya kwanza Azam FC kucheza na Mbao, hii inatokana na timu hiyo kupanda Ligi Kuu msimu huu ikiwa tayari imeshacheza mechi 14 za ligi, ikishinda mara tatu, sare nne na kufungwa saba.
Kikosi cha Azam FC kitacheza na Mbao kikiwa kimeimarika zaidi, baada ya kurejea kikosini kwa wachezaji wake watatu tegemeo waliokosa mechi zilizopita kwa sababu mbalimbali, beki Bruce Kangwa aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu ya mbavu yeye anatarajiwa kuwemo.
Beki kisiki Aggrey Morris, aliyeuokosa mchezo uliopita akitumikia adhabu ya kukusanya kadi tatu za njano, naye atakuwemo kikosini kuimarisha eneo la ulinzi, kama ilivyo kwa nahodha msaidizi Himid Mao, ambaye atarejea kuongeza nguvu eneo la kiungo cha ukabaji baada ya kukosa mechi mbili zilizopita akitumikia adhabu ya kadi nyekundu.
Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati Azam FC, wenye udhamini wa kinywaji safi cha Azam Cola kinachoburudisha koo na kuchangamsha mwili na Benki bora nchini kwa usalama wa fedha zako ya NMB, itaingia uwanjani bila uwepo wa wachezaji wake watatu ambao ni majeruhi.
Mabeki Shomari Kapombe, Daniel Amoah na mshambuliaji Shaaban Idd, aliyefunga bao la ushindi dhidi ya Toto African, ambaye amepata majeraha kwenye mazoezi ya mwisho leo asubuhi.
Tayari Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez na Nahodha John Bocco 'Adebayor', wamewahakikishia mashabiki wa timu kupigania pointi tatu katika mchezo huo huku wakizidi kuomba sapoti yao zaidi kuelekea mechi zijazo.
Ushindi wowote wa Azam FC leo utazidi kuiimarisha kwenye nafasi ya tatu inayoshika ikiwa na pointi 22 na kuzidi kuendeleza vita za kuwania ubingwa wa ligi hiyo.  
Mara baada ya mchezo huo, Azam FC inatarajia kukamilisha ng’we ya mzunguko wa kwanza wa ligi kwa kukipiga na Mwadui kwenye Uwanja wa Mwadui, Shinyanga Jumatano ijayo Novemba 9 mwaka huu, ukiwa ni mchezo wa kiporo.

No comments:

Post a Comment