tuwasiliane

Saturday, November 5, 2016

Mourinho akerwa na wachezaji wa Manchester United

Henrikh Mkhitaryan
Meneja wa Manchester United Jose Mourinho amesema wachezaji wa Manchester United walichukulia mechi dhidi ya Fenerbahce katika Europa League kana kwamba ilikuwa mechi ya kirafiki ya kujiandaa kwa msimu.
Red Devils walishuka hadi nambari tatu kwenye Kundi A ligi hiyo ndogo ya Ulaya baada ya kulazwa 2-1 na klabu hiyo ya Uturuki mjini Istanbul.
Manchester United sasa wameshinda mechi mbili pekee kati ya saba walizocheza mashindano yote karibuni.
"Timu inayofunga baada ya dakika mbili pekee ni timu ambayo haiko tayari, haijajiandaa kiakili, haina mwelekeo na haina umakinifu," amesema Mourinho.
United wamefunga mabao mawili pekee mechi zao nne walizocheza karibuni zaidi.
Aidha, walifungwa baada ya sekunde 30 pekee na Chelsea na sekunde 65 na Fenerbahce.
Mshambuliaji Moussa Sow alifunga kwa kombora la kushangaza la kupitishia mpira juu ya kichwa, naye Jeremain Lens akaongeza jingine kupitia frikiki kabla ya Wayne Rooney kufunga bao la kufutia machozi mechi ikikaribia kumalizika.
Bado lake hilo la dakika ya 89 limemuwezesha kufikia magoli 38 Ulaya na kufikia rekodi ya Ruud van Nistelrooy.
Hata hivyo, amefunga mabao mawili pekee katika mechi 17 alizocheza msimu wote.
Mourinho amesema: "Matatizo yetu yalianza na mtazamo wetu wa kiulimwengu. Walikuwa wanacheza fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, tulikuwa tunacheza mechi ya kirafiki ya majira ya joto. Huo ndio uhalisia wa jinsi mechi ilianza.
"Walistahili kushinda, soka haihusu tu ubora, kuna kutia juhudi pia, kujitolea, kujituma na kujitolea kabisa. Lazima ucheze dakika zote 90 kwa hamu na umakinifu.
"Katika mazingira kama haya, kuwapa nafuu wapinzani wako (kwa kufungwa mapema), hapo ndipo wanataka kuwa. Kisha, tulituliza kasi ya uchezaji na kuanza kumshinikiza refa, kuigiza kwamba tumechezewa vibaya na hayo ndiyo makosa yetu."
Meneja huyo wa zamani wa Chelsea hata hivyo alikiri kuwa "moja ya mambo mazuri leo ni kwamba Rooney hatimaye amefunga bao."Kati ya wachezaji walionunuliwa na Mourinho majira ya joto - Paul Pogba, Zlatan Ibrahimovic, Henrikh Mkhitaryan na Eric Bailly - ni Mfaransa Pogba pekee aliyeanza mechi.
Hata hivyo, aliondoka kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika akionekana kuumia.
Ibrahimovic aliiingia nafasi yake.
Mkhitaryan naye alichezeshwa mara ya kwanza tangu 10 Septemba. Aliingia dakika ya 61 nafasi ya Marcus Rashford. Beki wao Bailly anatarajiwa kukaa nje miezi miwili kutokana na jeraha la goti.
Haijabainika jeraha la Pogba ni mbaya kiasi gani na iwapo ataweza kucheza dhidi ya Swansea Ligi ya Premia Jumapili.

No comments:

Post a Comment