KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Jana asubuhi ilihamishia mazoezi yake ufukweni kwa kujifua vilivyo katika Fukwe za Coco Beach jijini Dar es Salaam.
Tokea Jumamosi iliyopita jioni, benchi la ufundi la Azam FC chini ya Kocha Mkuu Stewart Hall, limekuwa likiwafanyisha mazoezi ya nguvu wachezaji ili kuwaweka fiti na kuimarisha viwango vyao.
Programu hiyo ya jana ufukweni iliyochukua taktibani saa moja na nusu kuanzia saa 2 asubuhi, inakuwa ni programu ya mwisho kwa wachezaji kwa upande wa mazoezi ya nguvu.
Kwa mujibu wa Kocha Hall, leo asubuhi wataanza kujiandaa kimbinu zaidi uwanjani, ili kuweka matayarisho yao vizuri zaidi kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya African Sports utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi ijayo.
Akizungumza na mtandao wa azamfc.co.tz hivi karibuni, Hall alisema anawapa programu ya mazoezi ya nguvu wachezaji wake, ili kurudisha viwango vyao na kuiweka Azam FC kwenye ubora wake, ambao ulipotea katika michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Azam FC inayodhamini na Benki ya NMB, itaingia kwenye mchezo huo wa African Sports ikiwa na morali ya hali ya juu, hasa kutokana na wachezaji wake kuonyesha ari kubwa ya kujituma mazoezini na hamasa ya kushinda tokea walipoanza kujiandaa na mtanange huo.
Wakati huo huo, kikosi cha Azam FC leo asubuhi kinatarajia kuingia kambini kwenye makao makuu yake ya Azam Complex, Chamazi, jijini Dar es Salaam, kikiwa tayari kabisa kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya kuivaa African Sports.
Mabingwa hao wa michuano ya Kombe la Kagame mwaka jana waliojiwekea rekodi ya kulitwaa bila kufungwa mchezo wowote na kuruhusu wavu wake kuguswa, wanarejea kwenye patashika ya Ligi Kuu wakiwa kileleni mwa msimamo kwa pointi 35.
Hiyo ni baada ya kutofungwa mchezo wowote mpaka sasa kwenye mechi 13 za ligi walizocheza, ikishinda 11 na sare mbili walipocheza na Simba na Yanga.
Wakati Azam FC ikiwa kileleni, wapinzani wao African Sports wenyewe wanaburuza mkia kwenye msimamo wa ligi, wakwa na wamejikusanyia pointi saba tu baada ya kushinda mechi mbili, sare moja na kupokea vipigo michezo 10.
No comments:
Post a Comment