Yanga na Azam
Klabu za Yanga na Azam ndizo pekee zilizofanikiwa kupata fursa ya kushiriki michuano ya kimataifa kutoka Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Wawakilishi wa Tanzania bara kwenye michuano ya kimataifa klabu za Yanga na Azam FC huenda zikajua wapinzani wao kwenye michuano hiyo Desemba 15, kabla ya kuanza kwa michuano hiyo mapema Januari 2016.
Katibu mkuu wa Yanga Dk. Jonas Tiboroha, amekiambia chanzo chetu kuwa kutoka kwa ratiba hiyo kunawaongezea ari ya kuongeza bidii ya maandalizi kujiandaa na michuano hiyo ambayo wamedhamiria kufanya vizuri msimu huu.
“Hii ndiyo michuano mikubwa ambayo tumeilenga na hiyo inatokana na usajili tulioufanya msimu huu kwaiyo kutoka mapema kwa ratiba na kumjua mpinzani wetu kutatusaidia kujua mbinu mbadala za kutuvusha hatua inayofuata,”amesema Tiboroha.
Kwaupande wake Mtendaji Mkuu wa Azam Saad Kawemba, amesema hiyo itakuwa na unafuu mkubwa kwao kwai itakuwa imewapunguzia presha ya kujua ni timu gani wataanza nayo.
“Ninzuri kwetu kwasababu tutapunguza presha na kujua tujipange vipi ili tuweze kumkabili mpinzani wetu kwasababu michuano hiyo ni mikubwa na inaushindani wa hali ya juu,’amesema Kawemba.
Katika michuano hiyo Yanga itaiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuibuka mabingwa wa ligi ya Vodacom  msimu uliopita, huku Azam yenyewe ikiiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Shirikisho la soka Afrika CAF, linakutana Desemba 15 kupanga na kutoa ratiba hiyo itakayoainisha kila timu na mpinzani wake kwenye michuano hiyo.