Thursday, December 31, 2015
DILI LA SAMATTA ULAYA LAKAMILIKA KWA ASILIMIA 90
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amesema mpango wa kujiunga na KRC Genk ya Ubelgiji kwa asilimia 90 umekamilika.
Katika mazungumzo yake na Waziri wa Habari Vijana Wasanii na Michezo, Nape Nnauye leo Dar es Saaam, Samatta amesema kwamba kwa sasa kilichobaki ni klabu yake, TP Mazembe ya DRC kumalizana na Genk ili ahamie Ulaya.
“Tumefikia makubaliano ya awali na Genk na sasa kilichobaki ni TP Mazembe kumalizana nao ili nikajiunge nao. Naweza kusema kwa asilimia 90 mimi ni mchezaji wa Genk,”amesema Samatta ofisini kwa Waziri Nape jana.
Aidha, Samatta alisema kwamba amekwenda ofisi ya Waziri Nape kupata baraka za serikali kabla ya kwenda Nigeria kwenye sherehe za tuzo za Wanasoka Bora mwaka 2015.
Samatta ameingia fainali ya wachezaji watatu kuwania tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Afrika pamoja na kipa Robert Kidiaba anayecheza naye TP Mazembe ya DRC na Baghdad Boundjah wa Algeria na Etoile du Sahel ya Tunisa.
Katika tuzo ya Mwanasoka Bora wa Jumla wa Afrika, walioingia fainali ni Andre Ayew wa Ghana na Swansea City, Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon na Borussia Dortmund na Yaya Toure wa Ivory Coast na Manchester City, anayeshikilia tuzo hiyo.
Washindi wapatikana kutokana na kura zitakazopigwa na makocha wakuu wa timu za taifa au Wakurugenzi wa Ufundi wa Vyama na mashirikisho ya soka ya nchi zote wanachama wa CAF na watatangazwa katika usiku wa tuzo za Glo-CAF Januari 7 mwaka 2016.
Pamoja na hayo, Samatta amempongeza Nape kwa kuchaguliwa kuwa Waziri mpya wa michezo.
Kwa upande wake, Nape amempongeza Samatta kwa mafanikio yote, kuingia fainali ya tuzo za Mwanasoka Bora Afrika na kuwa mbioni kujiunga na Genk.
Samatta alijiunga na Mazembe mwaka 2012 akitokea Simba SC ya Dar es Salaam, ambayo aliichezea kwa msimu mmoja tu baada ya kujiunga nayo akitokea African Lyon, zamani Mbagala Market.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment