Klabu ya Yanga ipo hatarini kupoteza mamilioni ya
fedha kama fidia kutokana na kutothamini, kutoheshimu mikataba baina
yake na wadau mbalimbali wa soka ndani na nje ya nchi.
Uchunguzi wa gazeti hili unaonyesha kuwa mabingwa
hao wa kihistoria wa soka nchini wanaweza kulazimika kulipa fidia ya
zaidi ya Sh500 milioni kama watabainika wamekiuka mikataba yao na Benki
ya Posta, Emmanuel Okwi pamoja na klabu ya FC Lupopo.
Uongozi wa klabu hiyo leo unalazimika kuwasilisha
ushahidi mbele ya Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ya
Shirikisho la Soka Tanzania kabla ya kamati hiyo kuiamuru kumlipa Okwi
dola 50,000 (Sh81.1 milioni) anazoidai klabu hiyo.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, kamati hiyo ya TFF,
chini ya mwanasheria Richard Sinamtwa ilimtangaza Okwi kuwa mchezaji
huru baada ya Yanga kushindwa kutimiza matakwa ya mkataba.
Kutokana na hali hiyo, Yanga italazimika kumlipa
Okwi mishahara yake ya miezi sita sanjari na Sh81.1 milioni za
usajili. Okwi alikuwa kwa mwezi akipokea Sh4 milioni na kama kamati hiyo
ya sheria itaamuru Yanga kumlipa mshahara wake wote, basi italazimika
kumpa Sh24 milioni.
Mbali na Okwi, Yanga pia imejikuta ikiingia kwenye
mgogoro na timu ya FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
(DRC), ambayo inaidai klabu hiyo dola 15,000 ( Sh24.7 milioni).
Viongozi wa FC Lupopo wamewasilisha barua TFF
kuomba msaada ili walipwe fedha zao ambazo ni za usajili wa beki Mbuyu
Twite aliyetua Yanga akitokea APR ya Rwanda, huku Lupopo ikidai klabu
hiyo ya Twiga/ Jangwani kuwazunguka.
Kwa mujibu wa aliyekuwa ofisa habari wa TFF,
Boniface Wambura (sasa Mkurugenzi wa Mashindano), shirikisho hilo
linayo barua ya Lupopo na katika makubaliano ya Yanga na Lupopo, kuna
kipengele ambacho kinailazimisha Yanga kuwapa sehemu ya asilimia ya
fedha za usajili wa Twite.
Yanga kwa upande wake iliwalipa Lupopo dola 20,000
baada ya kumsajili Twite kwa mkataba wa miaka miwili uliomalizika msimu
uliopita na tayari beki huyo amesaini mkataba mwingine wa mwaka mmoja
na hivyo timu hiyo ya Jangwani walipaswa kuwalipa Lupopo dola 15,000,
kama mkataba unavyosema, lakini jambo hilo halijafanyika.
Pia, Yanga imeingia kwenye mgogoro wa kimkataba na
Benki ya Posta ambao walikubaliana kutengeneza kadi maalumu kwa ajili
ya wanachama, lakini hivi karibuni Yanga walisaini mkataba kama huo na
benki ya CRDB.
Meneja Uhusiano wa TPB, Noves Moses akizungumza
siku moja baada ya Yanga na CRDB kusaini mkataba huo alisema: “Yanga
walituletea notisi asubuhi ya kueleza nia yao ya kutoendelea nasi,
lakini baadaye tukasikia kupitia vyombo vya habari wameingia mkataba na
CRDB.
“Kwa ufupi, Yanga hawakufuata utaratibu kwa vile
walipaswa kutupa notisi ya miezi mitatu, lakini wao wametupa asubuhi na
siku hiyo hiyo wameingia mkataba na CRDB, kama kuna upungufu tungeweza
kujadiliana ni lazima sheria ichukue mkondo wake,” alisema.
Kundi lingine linaloidai Yanga ni waliokuwa watendaji wake;
aliyekuwa katibu mkuu wake, Celestine Mwesigwa na Louis Sendeu aliyekuwa
ofisa habari.
Septemba mwaka jana, watendaji hao waliondolewa
katika ajira zao kwa kile kilichoelezwa kuwa uongozi haukuridhika na
utendaji wao.
Mwesigwa na Sendeu waliomba bila mafanikio walipwe
na Yanga fidia ya Sh 262 milioni ambapo kati ya hizo, Sendeu anadai
Sh79 milioni na Mwesigwa, Sh 183 milioni.
No comments:
Post a Comment