Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu
wake (wakati huo ikiitwa FAT), Kanali mstaafu Ali Hassan Mwanakatwe
kilichotokea leo asubuhi (Juni 7 mwaka huu) katika Hospitali Kuu ya
Jeshi (GMH) Lugalo jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa binti wa marehemu,
Sophia, baba yake alianguka bafuni nyumbani kwake Mbezi Beach ambapo
alikimbizwa katika Hospitali ya Lugalo ambapo ndipo umauti ulipomfika
wakati madaktari wakimpatia matibabu.
Kanali Mwanakatwe alichaguliwa
kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) katika
uchaguzi uliofanyika mwaka 1993 mjini Kibaha mkoani Pwani.
Baada ya kuondoka FAT, aligombea
nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam
(DRFA) na kufanikiwa kushinda katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1997.
Msiba huo ni mkubwa katika fani
ya mpira wa miguu nchini na Afrika kwa ujumla kwani, Kanali Mwanakatwen
enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa akiwa kiongozi, na mkufunzi wa
utawala wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Pia aliwahi kuwa
Kamishna wa CAF.
TFF tunatoa pole kwa familia ya
marehemu Kanali Mwanakatwe, DRFA, na Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki
kigumu cha msiba huo mzito.
Taratibu za mazishi zinaendelea
kufanywa na familia yake nyumbani kwake Mbezi Beach karibu na hoteli ya
Giraffe wakati ndugu wakisubiriwa kutoka mikoani. TFF tunasubiri
taratibu hizo ili tujipange jinsi ya kushiriki katika msiba huo.
Sisi sote ni waja wake Mola. Hakika kwake tutarejea.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment