Kampuni ya Statoil ya Norway na mshirika wake ExxonMobil wamegundua kiasi kingine kikubwa cha gesi katika Bahari ya Hindi nchini Tanzania.
Kiwango hicho kinakadiriwa kufikia futi za ujazo trilioni mbili mpaka tatu (sawa na lita trilioni 56.6 hadi trilioni 84.9).
Ugunduzi huu unafanya jumla ya ujazo wa gesi
iliyogunduliwa na washirika hao kufikia takriban futi za ujazo trilioni
20 (lita trilioni 566.25) kwenye Kitalu Namba 2, ambako washirika hao
wanafanya shughuli za utafiti na uchimbaji.
‘’Tangu mwaka 2012 tumekuwa tukipata mafanikio ya
asilimia 100 nchini Tanzania na eneo hilo limekuwa kitovu cha utafiti
ndani ya muda mfupi. Ni kwa haraka tulitoka kwenye kuchimba kisima
kimoja hadi kuwa na mkakati wa kuchimba visima vingi,’’ alisema Makamu
wa Rais wa Shughuli za Utafiti za Statoil Ukanda wa Magharibi, Nick
Maden.
Ugunduzi huo mpya katika Kisima Piri-1 umefanyika
katika eneo lenye kiwango kidogo cha mawe ya mchanga kama ilivyokuwa
wakati ilipogunduliwa gesi katika Kisima cha Zafarani-1 mwaka 2012.
Ugunduzi katika kisima hicho unakuwa wa sita katika Kitalu Namba 2.
Uchimbaji wa gesi katika kisima hicho ulifanywa na
meli ya Discoverer Americas, usawa wa mita 2,360 za kina cha maji. Meli
hiyo sasa inachimba kisima kingine cha Binzari katika Kitalu namba 2.
“Eneo lingine la utafiti limeshaandaliwa na
litajaribiwa ndani ya mwaka 2014 na 2015. Tunatarajia kuchimba visima
zaidi na tunatumaini kuwa matokeo ya visima hivi yataongeza kiasi cha
ujazo wa gesi kwa ajili ya miundombinu ya mradi mkubwa wa gesi hapo
baadaye,’’ alisema Maden.
Statoil ambayo imekuwapo nchini tangu 2007,
inatafiti na kuchimba gesi katika kitalu namba mbili kwa niaba ya
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ikiwa na hisa ya
asilimia 65 katika kitalu hicho wakati ExxonMobil Exploration and
Production Tanzania Limited ina asilimia 35.
SOURCE.www.mwananchi.co.tz
SOURCE.www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment