
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara imeamua msimu ujao klabu zinazoshiriki ligi hiyo kusajili wachezaji watano wa kigeni badala ya wachezaji watatu.
Awali, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitaka
kupunguza usajili wa wachezaji wa kimataifa kutoka watano hadi watatu
ili kutoa nafasi kwa wachezaji wazawa kucheza zaidi.
Mabingwa wapya Azam tayari ina wachezaji watano
ambao ni Brian Umony (Uganda), mapacha Kipre Tchetche na Kipre Balou
(wote kutoka Ivory Coast) na hivi karibuni imesajili mshambuliaji kutoka
Mali, Ismailla Diarra kwa mkataba wa miaka miwili na Didier Kavumbagu
(Burundi) akichukua nafasi ya Mohamed Kone waliyemfungashia virago.
Taarifa za kubakisha wachezaji watano zitakuwa
shangwe kwa Yanga, ambao walidai kupokwa Kavumbagu kwa vile sheria mpya
ya TFF ya kutaka kubaki wachezaji watatu ndio iliyowabana na kusababisha
kushindwa kuwapa mkataba kwa wakati Kavumbagu na Mbuyu Twite, ambaye
usajili wake unasubiri maamuzi hayo.
Akizungumza kuwapo kwa taarifa za kubaki kwa
kipengele hicho, mmoja kati ya viongozi wa TFF, ambaye hakutaka jina
lake kuandikwa kwa kutokuwa msemaji, alisema Bodi ya Ligi imependekeza
kuwa na wachezaji watano kwa misimu mitatu mfululizo.
“Azam wanashiriki Ligi ya Mabingwa mwakani, halafu
Azam ni wadhamini wa Ligi Kuu Bara, kuna mambo mengi yameangaliwa
ikiwamo ligi yetu kuwa bado changa na wachezaji wa kigeni ndio wamekuwa
wakitoa changamoto na kuleta ushindani kwa wachezaji wetu wa ndani na
kuifanya ligi iwe angalau na mvuto,” alisema.
Hata hivyo, licha Bodi ya Ligi kupitisha
mapendekezo hayo, TFF ambao ndiyo wasimamizi wa mpira nchini watakutana
na klabu za Ligi Kuu Mei 11 na kuwaeleza maazimio ya Kamati ya Utendaji
ya TFF ambayo ilikaa jana, pia watajadili mikataba mbalimbali ya ligi na
kuangalia namna ya kuiboresha.
Pendekezo la kutumia wachezaji watatu katika ligi
msimu ujao lilikuwa ni utekelezaji wa Azimio la a Bagamoyo ambalo
limeonekana kuwa gumu kutekelezeka.
Mwaka 2007 TFF kwa ufadhili wa Shirikisho la Soka
la Kimataifa (Fifa) iliandaa semina mjini Bagamoyo ikishirikisha
viongozi wa klabu na wadau wa soka na kufikia makubaliano ya timu za
Ligi Kuu kuwa na idadi ya wachezaji wa kigeni wasiozidi watatu ili
kuwapa nafasi wazawa.
Pendekezo la timu za Ligi Kuu kuwa na wachezaji wa kigeni wasiozidi watatu lilipaswa kuanza kufanyiwa kazi msimu wa Ligi Kuu ya
Tanzania Bara uliomalizika hivi karibuni, lakini
ilishindikana baada ya baadhi ya timu kuomba kuongezwa muda wa msimu
mmoja kabla ya utekelezaji wake na hivyo lilitakiwa lianze kutumika
msimu ujao, ambapo pia limegonga mwamba.
Akizungumzia suala hilo la usajili wa wachezaji
watano wa kigeni, msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema: “Bado
hatujapata mwongozo wowote kutoka TFF licha ya kuomba, hata hivyo Mei 11
kuna kikao cha klabu za Ligi mambo yote yataamuliwa huko.”
Kwa upande wake, Meneja wa Azam FC, Jemedari Said, alisema:
“Suala hilo ni kubwa kwangu, viongozi wa juu ndio wanahusika nalo zaidi,
Jumatatu tuna kikao kule (TFF), ndio kila kitu kitajulikana.”
Katibu wa Simba, Ezekiel Kamwaga hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo.
source; www.mwananchi.co.tz
source; www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment