‘Ni machozi, jasho na damu, au unasema patashika nguo kuchanika,’ Yanga itakapojitupa uwanjani leo kuikabili Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Pambano hilo linasubiriwa kwa hamu kubwa na
mashabiki wa soka kutokana na mchezo huo kubeba hisia za mashabiki wengi
kutokana na upinzani mkali uliokuwepo kwenye mchezo wa awali uliochezwa
mkoani Mbeya.
Yanga ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na
pointi 32 wakati Mbeya City ni ya tatu ina pointi 31, huku Azam
wakiongoza kwa pointi 33.
Katika mchezo wa kwanza uliofanyika Septemba 14, mwaka jana, timu hizo zilitoka sare 1-1 katika Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Katika mchezo huo, mashabiki wa soka wa jiji la
Mbeya walituhumiwa kuvunja kioo cha basi la Yanga na kuzua mtafaruku
uwanjani hapo na Mbeya City kulazimika kuilipa Yanga Sh2 milioni.
Katika mechi mbili za kwanza za mzunguko huu,
Yanga iliifunga Ashanti 2-1, ikatoka suluhu na Coastal Union wakati
Mbeya City iliifunga Kagera Sugar bao 1-0 kisha ikatoka sare ya bao 1-1
na Ruvu Shooting.
Kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm alisema
anafikiri mchezo huo utakuwa mgumu, ingawa hajawahi kuiona Mbeya City
ikicheza uwanjani.
Mara baada ya kutoka Tanga, kikosi cha Yanga
kilielekea moja kwa moja Bagamoyo kuweka kambi na tayari kiungo wake
aliyekuwa amesimamishwa Athuman Idd ‘Chuji’ amerejeshwa kundini.
Mbeya City ilipomaliza mechi yake na Ruvu Uwanja
wa Mlandizi, Pwani ilielekea Morogoro kuweka kambi ya muda huku ikifanya
mazoezi Uwanja wa Jamhuri chini ya Kocha Juma Mwambusi ambaye alisema :
“Unajua mechi kama hii wachezaji huwa wanakamia sana sasa kazi yangu ni
kuwashusha presha waone mechi ya kawaida ili tushinde.” alisema.
Mechi nyingine leo ni ile ya vinara wa ligi Azam
dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex wakati Prisons
ikiendelea ‘kula bata’ baada ya mchezo wake dhidi ya Coastal Union
uliokuwa ufanyike leo kwenye Uwanja wa Sokoine kusogezwa mbele hadi
Februari 5 kupisha sherehe ya Miaka 37 ya Kuzaliwa CCM.
No comments:
Post a Comment