tuwasiliane

Monday, January 13, 2014

SIMBA YAWANIA NDOO YA MAPINDUZI LEO

 
TIMU ya soka ya Simba SC, leo inawania taji la 40 tangu ianzishwe mwaka 1936, wakati itakapomenyana na KCC ya Uganda katika Fainali ya Kombe la Mapinduzi, Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Timu hiyo maarufu kama Wekundu wa Msimbazi, ilianzishwa mwaka 1936, enzi hizo ikijulikana kwa jina la Queens, yaani Watoto wa Malkia, kabla ya baadaye kubadilisha jina na kuwa Eagles, yaani ndege aina ya Tai, jina ambalo halikudumu sana nalo likatupwa na kuwa Sunderland, ambalo lilidumu hadi mwaka 1971 lilipobadilishwa na kuwa Simba SC hadi leo.


Kiungo Amri Ramadhani Kiemba amefunga mabao matatu hadi sasa kwenye mashindano haya, anazidiwa bao moja tu na mchezaji anayeongoza, Owen Kasuule wa URA ya Uganda iliyotolewa na Simba SC katika Nusu Fainali.
Ramadhani Yahya Singano ‘Messi’ amecheza vizuri katika mechi zote nne alizopangwa na hadi sasa ni kati ya wachezaji wanaotazamiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa mashindano.
Wachezaji hawa watatu, Mapunda, Kiemba na Messi hakika leo wanatarajiwa kuwa chachu ya matokeo mazuri kwa Simba SC- mbele ya KCC yenye matumaini makubwa ya kuondoka na Kombe la Mapinduzi.  
Kampuni ya CXC Safaris & Tours ya Dar es Salaam, chini ya Mkurugenzi wake, Charles Hamkah inatarajiwa kutoa Sh. 300,000 kwa kila mmoja, mfungaji bora, mchezaji bora na kipa bora. 
Hii ni michuano ya nane ya Kombe la Mapinduzi inayokuja sambamba na sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar tangu kung’olewa kwa utawala dhalimu wa kisultani visiwani hapa. 
Timu tano zimetwaa Kombe hilo tangu limeanzishwa mwaka 2007, Yanga SC ya Dar es Salaam ikikata utepe, ikifuatiwa na watani wao, Simba SC (2008), Miembeni ya hapa (2009), Mtibwa Sugar ya Morogoro (2010), Simba SC tena 2011 na Azam FC mara mbili mfululizo 2012 na 2013.
Mabingwa watetezi, Azam safari hii wamekwama kwenye Nusu Fainali baada ya kutolewa na KCC kwa kufungwa mabao 3-2, ikitoka nyuma kwa 2-0. 

Katika mchezo wa leo, unaotarajiwa kuchezeshwa na refa mwenye beji ya FIFA, Ramadhani Ibada ‘Kibo’, vikosi vya timu zote vinatarajiwa kuwa; 
Simba SC; Ivo Mapunda, Haruna Shamte, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Donald Mosoti ‘Beki Adui’, Joseph Owino, Jonas Mkude, Haroun Chanongo, Amri Kiemba, Amisi Tmbwe, Ramadhani Singano ‘Messi’ na Awadh Juma.
KCC; Omar Magoola, Saka Mpima, Habib Kavuma, Ibrahim Kiiza, Fahad Kawooya, Gadafi Kiwanuka, Herman Wasswa, Tom Masiko, Tony Odur, Stephen Bengo na William Wadri.

No comments:

Post a Comment