tuwasiliane

Tuesday, September 10, 2013

Mwamuzi aliyechezesha Yanga, Coastal atimuliwa

 
YANGA imemponza mwamuzi, Martin Saanya wa Morogoro aliyechezesha mechi yao na Coastal Union ambaye amefungiwa mwaka mmoja kwa kuchezesha mchezo huo chini ya kiwango.
Saanya amepewa adhabu hiyo ya kutochezesha mechi yoyote ya soka ndani ya kipindi hicho sawa na mshika kibendera namba moja wa mechi hiyo, Jesse Erasmo ambaye alishindwa kutoa uamuzi sahihi wa adhabu ya penalti waliyopewa Coastal ndani ya dakika za nyongeza kabla ya mpira kumalizika na kusababisha sare ya bao 1-1.
Penalti hiyo ndiyo ilisababisha vurugu ambazo zilifanywa na mashabiki wa Yanga ambao , walimshambulia mwamuzi kwa chupa za maji na kuvunja kioo cha basi la wachezaji wa Coastal na kumjeruhi kichwani beki wa timu hiyo, Hamis Hamad aliyelazimika kuwahishwa hospitali.
Adhabu hizo zimekuja baada ya Bodi ya Ligi kupitia taarifa ya kamishna wa mechi hiyo, Omary Walii kutoka Arusha.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Silas Mwakibinga aliliambia CHANZO CHETU kuwa: “Saanya na Erasmo wamefungiwa mwaka mmoja kuchezesha mechi za ligi baada ya bodi kupitia ripoti ya kamishina wa mchezo huo.
Saanya ameadhibiwa kwa kuchezesha chini ya kiwango na alitoa adhabu ya penalti iliyofungwa na Coastal akiwa mbali na tukio,” alisema Mwakibinga na kufafanua kuwa posho za waamuzi wa mechi kwa sasa ni Sh 250,000 mbali na nauli na teksi tofauti na zamani walipokuwa wanalipwa shilingi 170,000.
“Kwa upande wa Erasmo ndiye alikuwa eneo la tukio ilipotokea penalti, lakini alishindwa kumsaidia mwamuzi wa kati na kubaki ameduwaa kama asiye na uhakika.”
Mwakibinga alisema mbali na adhabu hizo kwa waamuzi, Kamati imemfungia kocha wa makipa wa Coastal Union, Juma Pondamali muda wa miezi mitatu na faini ya Sh1 milioni kwa kutoa lugha ya matusi kwa mashabiki wanaodaiwa ni wa Simba.
Katika hatua nyingine, Coastal imetozwa faini ya Sh100,000 kwa kuchelewa kikao cha maandalizi ya mechi asubuhi kwa dakika 23 huku Yanga ikitozwa faini ya Sh1 milioni kwa mashabiki wake kurusha chupa uwanjani na pia kumvamia mwamuzi huku viongozi wakishindwa kuwadhibiti.
Kuhusu basi la Coastal hakukuwa na taarifa kwani tukio lilitokea nje ya uwanja.

No comments:

Post a Comment