tuwasiliane

Tuesday, September 10, 2013

Kaniki,Matumla wanaswa na unga


STRAIKA wa zamani wa Simba, Joseph Kaniki ‘Golota’ pamoja na bondia chipukizi, Mkwanda  Matumla wapo mikononi mwa polisi jijini Addis Ababa, Ethiopia kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya.
Watuhumiwa hao wawili, raia wa Tanzania ambao wanajuta na kububujikwa na machozi kila kukicha walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Jumatatu iliyopita kwenye eneo linaloitwa Arada. Siku yoyote kuanzia leo Jumanne watapanda kizimbani tena kwa mara nyingine.
Mwanaspoti liliipata habari hii tangu Jumamosi jioni na kuanza kuifanyia kazi kabla ya Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia, Samuel Shelukindo kuithibitishia Mwanaspoti jana  Jumatatu kwamba wanamichezo hao wameshikiliwa nchini humo na polisi wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Jinai.
Wanamichezo hao walikamatwa na kilo saba za dawa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole jijini Addis Ababa, Mkwanda akikutwa na kilo nne wakati Kaniki alikuwa na kilo tatu.
Walikuwa wanajiandaa kuunganisha ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia wakielekea Paris, Ufaransa.
“Wameshikiliwa hapa Ethiopia kwa zaidi ya siku 10 sasa, sisi tulipigiwa simu na polisi wa hapa Alhamisi kujulishwa kwamba kuna Watanzania wawili wameshikiliwa kwa tuhuma za kukutwa na madawa ya kulevya, tulipokwenda tukamkuta ni Kaniki na Matumla,” alisema Shelukindo.
“Wao wenyewe wanaeleza kwamba walipitia Mombasa na huo mzigo walipewa na mtu mmoja wao walikuwa hawaelewi ukoje. Lakini Kaniki yeye anajitetea kwamba huyo aliyewapa huo mzigo pale Mombasa anajuana vizuri na Mkwanda. Kwa hiyo alichofanya yeye ni kuubeba tu, walikuwa wapite hapa Addis wakashuke Paris, Ufaransa ndio warudi Sweden kwa njia zao wanazojua wenyewe. Walipofika hapa Mkwanda alifanikiwa kupenya akapanda ndege lakini Kaniki akanaswa na mbwa ndipo akajitetea kwa polisi kwamba lile begi lilikuwa lake lakini mizigo mingine ilikuwa ya Mkwanda.
“Ndio hapo sasa Mkwanda akashushwa kwenye ndege wakashikiliwa na Jumatatu ya wiki iliyopita wakapandishwa kwenye Mahakama ya hapa kutajiwa kesi yao lakini hawakupewa nafasi ya kujitetea, hiyo kesi itatajwa tena Jumanne (leo) na Jumatano (kesho) na uchunguzi wa Polisi bado unaendelea.
“Kilichotokea ni jambo la aibu kwa nchi na hata wachezaji wenyewe wanajuta kwa mfano Kaniki anasema alikuwa aende England kucheza mpira mwezi Desemba lakini sisi tukamwambia hatuwezi kumsaidia inabidi akabiliane na kesi iliyoko mbele yake. Mkwanda yeye ametuambia kwamba anaishi Sweden hatuna maelezo yake zaidi,”alisema Shelukindo na kuongeza kuwa wamewapelekea wanamichezo hao msaada wa mablanketi kwa vile bado wako mahabusu na kwamba Ethiopia kwa sasa ni baridi kali.
Shelukindo alisema kwamba wachezaji hao wanaishi mahabusu kwenye kituo cha polisi (Federal Police Crime Investigation) na hawana chochote zaidi ya nguo walizokuwa wamevaa.
Alisema kuwa uwezekano wa Kaniki na Matumla kuachiwa au kesi yao kurudishwa Tanzania haupo kwa kuwa nchi hizi mbili hazina utaratibu wa kubadilishana wafungwa.
Shelukindo alisema pia Watanzania wengine waliokumbwa na madai kama yao walihukumiwa nchini Ethiopia.

“Kuna Watanzania wengine walinaswa hapa miaka ya nyuma wao walikuwa wamemeza wakapasuliwa yakatolewa na baadhi yao walifariki, hao wanne ambao wamemaliza vifungo vyao vya miaka minne wanaweza kurudishwa Tanzania muda wowote kuanzia sasa lakini kwa kesi kama hizi kifungo chake kama wakikutwa na hatia inakuwa ni miaka tisa mpaka 15.”
Wanamichezo hao inasemekana walikabidhiwa mizigo hiyo baada ya kupita sehemu zote za ukaguzi kwenye Uwanja wa Ndege wa Mombasa, Kenya.
“Walipewa mizigo hiyo wakati wakifanya taratibu za kupewa pasi ya kupandia ndege. Walipewa mizigo hiyo na huyo mtu na wakagongewa mihuri na ndio wakaelekea kwenye ndege,” kiliongeza chanzo chetu.
Mtu huyo aliwaomba wamsaidie kubeba mizigo ya dada yake, ambaye anaishi Sweden. Wanamichezo hao waliwaeleza maofisa ubalozi wa Tanzania huko Ethiopia kuwa hawakuwa wanafahamu kilichokuwemo ndani ya begi hilo.
Hata hivyo, Shelukindo alisema mzigo huo ulikuwa umeshindiliwa chini kabisa ya mabegi yao

No comments:

Post a Comment