tuwasiliane

Friday, June 14, 2013

Ibada ya siku tatu kuiombea Taifa Stars



Askofu Mkuu wa Kanisa la Good News For All Ministry,  Charles Gadi  PICHANI, kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa dini, leo wameandaa ibada maalumu ya maombi ya wazi ya timu ya Taifa, ‘Taifa  Stars’ ili iweze kuibuka na ushindi kwenye mchezo dhidi ya Ivory Coast  kesho kwenye Uwanja wa Taifa.
Gadi aliwataka Watanzania kuungana pamoja kuiombea timu hiyo, kwani  haijawahi kufika mbali katika mchezo ya kimataifa.
“Tuna imani timu yetu ni nzuri, lakini inahitaji maombi zaidi kwa kuwa inacheza na timu ngumu,” alisema askofu Gadi.
Aliitaka jamii iendelee kufanya maombi na kuhamasisha misaada ya hali na mali kwa timu hiyo.
Wakati huohuo, Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen amewapa wachezaji wake mbinu mpya ya kuwakabili nyota wa Ivory Coast katika mchezo wa kuwania  tiketi ya kufuzu Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil.
Poulsen alisema kubwa alilowafundisha wachezaji wake ni kujiamini  watakapokuwa wakicheza na miamba hiyo ya soka Afrika. “Nimewaambia  wachezaji wajiamini, wasicheze na majina ya wapinzani wao,” alisema  Poulsen.
“Ivory Coast ni timu bora, lakini nimewataka wachezaji wangu waione  kama timu ya kawaida kwenye mchezo wa Jumapili. Jambo la msingi wacheze  kwa kujiamini,” alisema Poulsen.

No comments:

Post a Comment