KAMA
ni harusi, tayari Yanga wametoa mahari na sasa wanasubiri kwenda
kufunga ndoa Mei 1, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumbeba
mwali wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Hiyo
inafuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Taifa, hivyo
kutimiza pointi 56 na sasa inahitaji pointi tatu zaidi katika mchezo
wake ujao dhidi ya Coastal Union ya Tanga ili rasmi kubeba ubingwa,
ulioachwa wazi na waliokuwa watetezi, Simba SC.
Pamoja
na ushindi, Yanga SC leo iliwapa burudani nzuri mashabiki wake kwa soka
maridadi ya kuonana kwa pasi za aina zote, ndefu na fupi, tena kwa
staili zote hadi visigino.
Katika
mchezo huo uliochezeshwa na refa Orden Mbaga, hadi mapumziko, Yanga SC
walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Simon Msuva, ambaye
alifunga kwa ustadi wa hali ya juu.
Mpira
uliozaa bao hilo ulianzia kwa Mbuyu Twite ambaye alimrushia mfungaji
akawahadaa mabeki wa JKT Ruvu na kuingia kwenye ‘sita’ akifanya kama
anataka kutoa pasi, lakini akafumua shuti kali moja kwa moja kufunga.
Hata
hivyo, baada ya bao hilo, wachezaji wa JKT Ruvu walimfuata mshika
kibendera namba mbili, Lulu Mushi wakilalamikia bao hilo, wakidai
lilitokana na maamuzi yasiyo ya haki ya mdada huyo.
Walilalamika mpira waliopewa Yanga warushe walistahili kurusha wao, JKT kwani aliyeutoa ni mshambuliaji wa Yanga, Hamisi Kiiza.
Kipindi
cha pili, Yanga SC walirudi na moto zaidi na kufanikiwa kupata mabao
mawili zaidi, yaliyofungwa na Hamisi Kiiza dakika ya 59 na Nizar Khalfan
dakika ya 64.
Kiiza
alifunga kwa kichwa akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na David
Luhende, baada ya Nizar Khalfan kuchezewa rafu nje kidogo ya eneo la
hatari.
Nizar
yeye alifunga baada ya kuuwahi mpira uliogonga mwamba na kurudi baada
ya Frank Domayo kuunganisha krosi ya Haruna Niyonzima.
Katika
mchezo wa leo, Yanga SC iliongozwa na kocha wake Msaidizi, Freddy Felix
Minziro ambaye alisema bosi wake, Mholanzi, Ernie Brandts anaumwa
Malaria.
JKT
iliendelea kuongozwa na Kocha Msaidizi, Azishi Kondo na kocha mpya,
Kenny Mwaisabula aliyetarajiwa kuanza kazi leo, hakuonekana uwanjani.
Kikosi
cha Yanga SC leo kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’/Said Mohamed dk 86,
Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan,
Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Haruna Niyonzima, Nizar
Khalfan/Said Bahanuzi dk90, Hamisi Kiiza/Jerry Tegete dk82 na Simon
Msuva.
JKT
Ruvu; Shaaban Dihile, Hassan Kikutwa/Sosstenes Manyasi dk77, Stanley
Nkomola, Ramadhani Madenge, Damas Makwaya, Nashon Naftali, Amos Mgisa,
Ally Mkanga/Charles Thadei dk78, Mussa Mgosi, Zahor Pazi na Haroun
Adolph.
No comments:
Post a Comment