tuwasiliane

Sunday, March 10, 2013

SIMBA YAFUNGIWA HOTELINI KABLA YA MECHI NA COASTAL

MENEJA wa Simba SC, Moses Basena, kipa Abbel Dhaira na kiungo Mussa Mudde, wote raia wa Uganda, wamefukuzwa kwenye hoteli ya Spice, Kariakoo, Dar es Salaam usiku huu kutokana na klabu hiyo kulimbikiza deni la Sh. Milioni 27.
Pamoja na kufukuzwa kwa Waganda hao usiku huu, uongozi wa Spice Hotel unashikilia magari mawili ya Simba SC, basi dogo na gari la kocha, aina ya GX110 hadi ulipwe fedha zake.
Kutokana na kufukuzwa Spice, Waganda hao walikwenda kuomba hifadhi katika hoteli ya Sapphire, ambako imeelezwa wamepokelewa na kupewa vyumba vitatu.    
Kocha Mfaransa, Patrick Liewig pekee ameachwa aendelee kuishi katika hoteli ya Spice. 
Mapema mchana wa leo, uongozi wa hoteli ya Sapphire Court, iliyopo Kariakoo pia, uliwazuia hotelini wachezaji wa Simba SC waliokuwa kambini hotelini hapo, ukishinikiza kulipwa deni la Sh. Milioni 25.7.
Simba SC ilizuiwa ikiwa inajiandaa kwenda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Hata hivyo, baadaye kaimu Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itangare ‘Kinesi’ alikwenda kuzungumza na wamiliki wa hoteli hiyo na kufikia mwafaka wa kulipa baada ya mechi ya Coastal.

Hati ya kusafiri ya Mtawala iko bondi Sapphire

Hati aliyosaini Mtawala kuahidi kulipa deni
Katibu wa Simba SC, Evodius Mtawala amesaini hati ya kuahidi kulipa deni hilo baada ya mechi ya leo na kuweka hati yake ya kusafiria kama bondi. Bado Menejimenti ya Sapphire inasistiza kulipwa fedha zake, vinginevyo itachukua hatua za kisheria dhidi ya klabu hiyo.   
Hamkani si shwari sasa ndani ya Simba SC, kufuatia viongozi wawili wa Kamati ya Utendaji, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Zacharia Hans Poppe kujiuzulu wiki hii.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage yuko India kwa matibabu na Kinesi aliyeteuliwa kukaimu Umakamu Mwenyekiti, sasa ndiye anakaimu Uenyekiti wa klabu.
Aidha, Baraza la Wazee kwa pamoja na Baraza la Wadhamini, wameunda Kamati Maalum ya kusimamia timu kuhakikisha inafanya vizuri katika wakati huu mgumu, chini ya Mwenyekiti, Rahma Al Kharoos, maarufu kama Malkia wa Nyuki.

No comments:

Post a Comment