| OPRAH Winfrey |
OPRAH Winfrey ni mwanamama bilionea aliyezaliwa Januari 29, 1954 huko, Kosciusko, Mississippi na kupewa jina la Orpah ambalo limo kwenye, Biblia katika Kitabu cha Ruth.
Jina la Orpah liliandikwa kimakosa katika cheti cha kuzaliwa na kusomeka Oprah ambalo limeendelea kuwa jina lake hadi sasa.
Oprah sasa ni kati ya wanawake matajiri duniani ambaye ukiichambua historia yake unakutana na matukio ya kusikitisha na kukatisha tamaa aliyokumbana nayo kabla ya kuwa bilionea.
Mikasa ya Oprah inaanzia katika mateso ya kifamilia, mama yake, Vernita Lee alikuwa masikini aliyetengana na mumewe huku kipato chake kikitokana na kazi ya utumishi wa ndani ambacho hakikutosha kuendesha maisha yake na ya mwanawe.
Oprah alizalimika kuishi na bibi yake, Hattie Mae Lee ambaye pia alikuwa masikini. Umasikini huo ulimfanya Oprah kuvaa nguo zilizoshonwa kwa magunia ya viazi na kuwa kituko kwa watoto wenzake mtaani.
Umewahi kuibuka mjadala kuhusu nani hasa baba mzazi wa Oprah kati ya Vernon aliyekuwa mwanajeshi wakati Oprah anazaliwa na Noah Robinson, mkulima aliyepigana vita ya pili ya dunia.
Akiwa na miaka mitatu, bibi yake alimfundisha kusoma na kwenda naye katika kanisa dogo na kadri siku zilivyokwenda alionyesha uwezo na kupewa jina la utani la "The Preacher" kutokana na umahiri wake wa kuchambua vifungu katika Biblia.
Hata hivyo bibi yake anakumbukwa zaidi kwa ukali, alikuwa akimchapa viboko aliposhindwa kusoma Biblia kwa usahihi au alipofanya kosa lolote.
Wakati Oprah akiwa kwa bibi yake, mama yake alijifungua mtoto wa pili wa kike, Patricia (marehemu), baadaye mama huyo alijifungua mtoto wa tatu pia wa kike.
Watoto hao wote walizaliwa mwanzoni mwa miaka ya 1960 na mama yake kulazimika kumtoa mtoto wake wa tatu akalelewe na familia nyingine kutokana na ugumu wa maisha.
Cha ajabu ni kwamba ingawa mtoto huyo wa tatu alizaliwa miaka ya 1960 lakini Oprah alijua kuhusu ndugu yake huyo mwaka 2010.
Pamoja na ugumu wa maisha, mama yake Oprah alijifungua mtoto mwingine wa nne, Jeffrey ambaye naye kwa sasa ni marehemu.
Yote tisa, Oprah mwenyewe akiwa na miaka tisa alidhalilishwa kijinsia na binamu, mjomba na marafiki wa familia, aliwahi kuwahadithia ndugu na jamaa zake matukio hayo lakini hawakuamini.
Akiwa na miaka 13 alikimbia kwao kutokana na kudhalilishwa kijinsia ikiwamo kubakwa na akiwa na miaka 14, alipata ujauzito na kujifungua mtoto wa kiume aliyefariki muda mfupi baada ya kuzaliwa.
Baadaye alilalamika kwamba familia yake ilimtapeli kwa kuuza habari hiyo katika Jarida la National Enquirer mwaka 1990.
Akiwa shule ya sekondari aliingia katika uhusiano wa kimapenzi na Anthony Otey, Oprah alimpenda mno Anthony na wakapanga kuwa mke na mume.
Hata hivyo Anthony baadaye alibaini kwamba Oprah alikuwa na malengo makubwa na hadhi ambayo yeye asingeweza kuifikia hivyo akaamua kuachana naye Siku ya Wapendanao.
Oprah mwenyewe aliwahi kusema kwamba hakuwa tayari kuwa mama kwa sababu hakupata malezi mazuri kwa mama yake.
Pamoja na kadhia zote na umasikini alipambana akasoma hadi Chuo Kikuu na kwa wakati wote alikuwa mwanafunzi bora na mwenye uwezo hususan katika kujieleza.
Mateso na kadhia zote vinabaki historia, ukimzungumzia Oprah leo hii unamzungumzia tajiri wa kutisha aliyetajirika kutokana na vipindi vyake maarufu kwenye Televisheni vya Oprah Winfrey Show.
Kilichomtajirisha ni kitu kilichotabiriwa na bibi yake aliyebaini uwezo wa Oprah kujieleza mbele ya halaiki na haikushangaza alipowekeza katika taaluma ya uandishi wa habari.
Miaka ya 1980 mwishoni ni wakati ambao The Oprah Winfrey Show kilikuwa juu Marekani na duniani kote, ni kipindi kilichojadili matukio na adha zinazowakumba watu mbalimbali.
Ingawa amewahi kuigiza filamu kadhaa na kuchapisha jarida lakini kipindi cha The Oprah Winfrey Show ndicho kilichompa utajiri.
Alianza kuupata utajiri huo akiwa na miaka 32 kipindi chake kilipoanza kuonyeshwa kote nchini Marekani na hadi anafikisha umri wa miaka 41 utajiri wake ulifikia Dola 340 milioni.
Hadi mwaka 2008 pato lake kwa mwaka liliongozeka na kufikia Dola 275 milioni.
Kwa mujibu wa Jarida la Forbes hadi Septemba 2010, utajiri wa Oprah ulifikia Dola 2.7 bilioni.
Oprah anaishi katika jumba la kifahari lililopo Montecito, Carlifonia, jumba lililopo kwenye eneo la ekari 42 linalofahamika kwa jina la "The Promised Land", (nchi ya ahadi).
Mbali na hilo lakini ana majumba mengine, New Jersey, Chicago, Kisiwa cha Island, Florida, Douglasville, Colorado, Maui, Hawaii na Antigua huku akidaiwa kumiliki ndege binafsi.

No comments:
Post a Comment