Takriban watu kumi na saba mpaka sasa wamethibitishwa kufariki baada
ya jengo lenye ghorofa zaidi ya kumi kuporomoka mjini Dar es Salaam,
Tanzania.
Waokozi wanaendelea na shughuli ya kuwatafuta na
kuwaokoa manusura na wanasema kuwa hadi sasa watu kumi na watatu
waliokuwa wamenaswa wameokolewa.Zaidi ya wengine sitini wangali wamenaswa chini ya vifusi.
Shughuli ya ujenzi ilikuwa inaendelea kwenye jengo hilo wakati lilipoporomoka katikati mwa mji wa Dar es Salaam.
Miongoni mwa watu ambao wangali kupatikana ni wafanyakazi wa mjengo na watoto kutoka shule jirani ya mafunzo ya dini ya kiisilamu.
Kulingana na walioshuhudia ajali hiyo, watu walisikika wakipiga mayowe kutaka msaada.
"nilidhani lilikuwa tetemeko la ardhi, na kisha nikasikia mayowe,'' alisema shahidi mmoja.
Jengo hilo liko katikati mwa Dar es Salaam na liliporomoka saa tatu kasorobo asubuhi kwa saa za Afrika mashariki.
Mamia ya watu wanaaminika kuwa ndani ya jengo hilo huku wengine wakiwa nje wakati wa ajali hiyo . Hata hivyo idadi kamili ya watu hao bado haujulikani.
Viongozi wamiminika
Rais Jakaya Kikwete alifika katika eneo la tukio
saa 6:45 mchana na alipata maelezo mafupi ya tukio hilo kutoka kwa Mkuu
wa Mkoa, Said Meck Sadik na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Suleiman Kova.
Baada ya maelezo hayo, Rais Kikwete aliyetumia
dakika tisa, alimwambia Mkuu wa Mkoa na Kamanda Kova: “…mmiliki na
mhandisi lazima wakamatwe mara moja.”
Kikwete baadaye alitikisa kichwa kuonyesha masikitiko na kuondoka.
Viongozi wengine waliofika ni Makamu wa Rais, Dk
Mohammed Gharib Bilal ambaye hata hivyo hakuzungumza lolote hata baada
ya kupata taarifa kutoka kwa mkuu wa mkoa.
Naye aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa (UN) ambaye sasa ni Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa
Kimataifa wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro alisema tukio hilo linaumiza na
kusikitisha kwani limepoteza nguvu kazi ya taifa.
“Ni vigumu kupata maneno ambayo yatabeba uzito wa
tukio hili lakini wajenzi wanatakiwa kuwa makini na ujenzi wao,” alisema
Migiro.
Wananchi wajitokeza kuokoa
Mapema Wananchi waliojitokeza kwa kushirikiana na
askari polisi na mgambo wa Jiji walioanza kuondoa kifusi cha mchanga kwa
kutumia mikono kutokana na kutokuwapo kwa vifaa vya kuondolea kifusi
hicho.
Ilipofika saa 4.30 ndipo trekta (kijiko) moja lilifika na
kushirikiana na wananchi ingawa halikuweza kuhimili kazi hiyo nzito na
kuhitajika trekta maalumu la kubeba na si kuzolea ili kunusuru uwezekano
wa kuhatarisha uhai wa waliofukiwa na kifusi.
Naibu Meya wa Halmashauri ya Ilala, Kheri Kessy
alisema,mwaka 2007 walitoa kibali kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC)
kwa kushirikiana na ‘Ali Raza Investment Limited’ kujenga jengo la
ghorofa 10.
“Kibali tulichotoa sisi ni cha kujenga ghorofa 10
na mkaguzi wetu alikuwa anafuatilia kila hatua hadi ilipofika ghorofa ya
10 akawa amemaliza kazi yake,” alisema Kessy.
Alipotakiwa kueleza kwanini hawakuchukua hatua
baada ya kuendelea kujengwa hadi kufikia ghorofa zaidi ya 16 alisema,
wao kwa hilo hawahusiki ila kuna taasisi zingine za Serikali
zinazosimamia majengo zinatakiwa kuulizwa.
“Kama nilivyosema,sisi tulitoa kibali cha kujenga
ghorofa 10 na mkaguzi wetu alikagua hadi ghorofa ya 10 hivyo kama
waliendelea kujenga sisi hatujui kwani kuna CRB (Bodi ya Usajili wa
Makandarasi) au ERB (Bodi ya Usajili ya Wahandisi) wao ndio wanahusika
zaidi watawaelezeni,” alisema Kessy.
NHC yatoa maelezo
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jana lilitoa
taarifa yake kuhusu tukio hilo na kueleza kuwa mradi wa ujenzi wa
ghorofa hilo ulikuwa ukifanyika kwa ubia kati yake na Kampuni ya Ujenzi
ya Ladha ya jijini Dar es Salaam, ambapo NHC lilikuwa na ubia wa
asilimia 25.
Ilieleza kuwa mbia huyo alipaswa kabla ya kuanza
ujenzi kupata vibali kutoka kwenye mamlaka husika na kuwa na wataalam wa
ujenzi na washauri waliokubalika na kuthibitishwa na mamlaka husika,
kwani NHC ilitoa ardhi tu kwa ajili ya ujenzi huo na ubia ungekamilika
mara baada ya jengo hilo kumalizika kujengwa.
“Mbia akishapata wataalam hao yeye ndio
anayehusika kuingia nao mikataba ya kazi ya kujenga na kusimamia ubora
wa jengo husika kwa mujibu wa sheria” ilieleza taarifa hiyo.

No comments:
Post a Comment