tuwasiliane

Wednesday, March 13, 2013

KIKOSI KIPYA CHA TAIFA STARZ,CHA KUIKABILI MOROCO

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mdenmark Kim Poulsen ametaja wachezaji 23 watakaoingia kambini Jumamosi wiki hii mjini Dar es Salaam kujiandaa na mechi ya Kundi C, dhidi ya Morocco kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil, ambayo itachezwa Machi 24 mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika kikosi hicho, Pulsen ameendelea kuwaita mabeki Aggrey Morris na Erasto Nyoni waliosimamshwa Azam FC tangu Novemba mwaka jana na hawajacheza mashindano yoyote mwaka huu. 
Mchezaji mpya ni kipa Hussein Sharrif ‘Casillas’ wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, ambaye ameonyesha umahiri mkubwa msimu huu akiwa na Wakata Miwa hao wa Manungu, tofauti na matarajio ya wengi kwamba Ally Mustafa 'Barthez' baada ya kudaka vizuri mfululizo Yanga, angeongeza orodha ya makipa wa Stars.
Kwa mujibu wa Kocha Kim, wachezaji wa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager wanatakiwa kuripoti kambini katika hoteli ya Tansoma, iliyopo eneo la Gerezani, Dar es Salaam Machi 17 mwaka huu.
Wachezaji walioitwa ni makipa Juma Kaseja kutoka Simba ambaye pia ndiye Nahodha wa Stars, Aishi Manula (Azam), Hussein Shariff (Mtibwa Sugar) na Mwadini Ally (Azam). 

Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Nassoro Masoud Cholo (Simba) na Shomari Kapombe (Simba).

Viungo ni Salum Abubakar (Azam), Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).

Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Mbali ya Kim, benchi la ufundi la Taifa Stars linaundwa na Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso (Meneja), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda (Mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).

Stars bado ina nafasi ya kukata tiketi ya Brazil mwakani, kwani hadi sasa inashika nafasi ya pili kwenye kundi lake, kwa pointi zake tatu nyuma ya Ivory Coast inayoongoza kwa pointi zake nne.

Hadi sasa, Stars imecheza mechi mbili, imeshinda moja nyumbani dhidi ya Gambia 2-1 na kufungwa moja na Ivory Coast ugenini 2-0.

Morocco wanashika nafasi ya tatu kwa pointi zao mbili, wakati Gambia yenye pointi moja inashika mkia na timu zote katika kundi hilo zimecheza mechi mbili mbili kila moja.    Wakati huo huo; Semina elekezi kwa ajili ya michuano ya Copa Coca-Cola 2013 itafanyika Machi 19 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Washiriki wa semina hiyo wanatakiwa kuripoti Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) siku moja kabla (Machi 18 mwaka huu).

Washiriki hao ni makatibu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar. Pia waratibu wa mikoa wa mashindano ya Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA).
Barua za mwaliko kwa ajili ya semina hiyo tayari zimetumwa kwa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa.

No comments:

Post a Comment