Serikali ya Uingereza hatimaye imeshindwa katika dakika za mwisho
kwenye kesi ya kumuondosha nchini hapa mhubiri wa dini ya kiislamu
mwenye itikadi kali Abu Qatada kwenda nchini Jordan
Abu Qatada amekuwa akitakiwa na serikali ya Jordan baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya ugaidi mwaka 1999.
Serikali ya Uingereza,imekuwa ikijaribu
kumuondoa nchini Uingereza,kiongozi huyo ambaye ni mhubiri wa dini ya
kiislamu kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita bila mafanikio,baada ya
mabishano makubwa ya kisheria.
Hili limekuwa ni anguko jingine kwa Serikali ya
Uingereza hasa wizara ya mambo ya ndani, ambapo Mhubiri huyo wa dini ya
Kiislamu anayetambulika kisheria kama Omary Mohammed Othman,maarufu kama
Abu Qatada,ameendelea kupata kinga ya mahakama ya kusalia nchini
Uingereza.
Mahakama ya rufaa mjini London,kwa pamoja
imeyakataa maombi ya Waziri wa mambo ya ndani Theresa May,ambaye
alipeleka kesi kwa niaba ya Serikali kuomba kumuondosha Abu Qatada
ambaye alipata kinga ya mahakama ya kusalia nchini Uingereza mwaka
uliopita.
Mahakama hiyo imesema kuna hatari kubwa kwa Abu
Qatada kupata mateso makali iwapo atakwenda kwenye mahakama za
Jordan,kulingana na makosa ya Ugaidi ambayo amekuwa akituhumiwa
kuyafanya.
Licha ya Mahakama hiyo kukubali kuwa Abu Qatada
ni mtu hatari sana,lakini hakuna usahidi wowote chini ya sheria za haki
za binadamu zinazoruhusu kumuondosha na kumpeleka nchini Jordan.
Serikali sasa,itaibidi itunge sheria kali
zitakazo iwezesha kuwaondoa nchini Uingereza watuhumiwa wa makosa ya
Ugaidi bila kujali amri ya mtu yeyote jambo ambalo linaonekana kuwa gumu
sasa.
Hata hivyo Wizara ya mambo ya ndani ya hapa
Uingereza,Imesema huu sio mwisho wa mapambano hayo ya kisheria,kwani
bado watakaa chini kutafakari na kushirikiana na Jordan kuangalia namna
ya kumuondosha hapa nchini kisheria bwana Abu Qatada.
SOURCE; BBC

No comments:
Post a Comment