TRA WAJIPANGA KUCHUKUA KODI KWA WAMILIKI WA NYUMBA
TRA wajiandaa wenye nyumba za kupanga sasa walipe kodi
UONGOZI wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wamesema wanakuna vichwa
juu ya jinsi ambavyo watafanikisha kukusanya kodi kutoka kwa wenye
nyumba nchini wanaofanya biashara ya kuzipangisha.
Kamishna
Mkuu wa TRA, Harry Kitillya alisema jijini hapa mwishoni mwa wiki kwamba
kuna changamoto nyingi katika ukusanyaji wa kodi kutoka kwenye nyumba
zilizopangishwa.
...
Alisema ni kawaida kwa kila mtu anayepata fedha kihalali lazima alipe
kodi, lakini utaratibu wa kudai kodi kutoka kwenye nyumba
zilizopangishwa bado unatafutwa.
“Katika ukusanyaji wa kodi
changamoto ipo kwenye kukusanya kodi inayotokana na biashara ya
upangisaji, kwa sababu wenye nyumba wengine hawataki kuonyesha mikataba
halisi, lakini sasa tumepata wazo tofauti ambalo tunalifanyia kazi ni
kutafiti kwamba bei za nyumba za kupanga kulingana na eneo husika, mfano
tukijua Masaki wanapangisha nyumba kwa kiasi gani tutakuwa tumepata pa
kuanzia, pia tunataka kulifanya suala hili kwa kuhakikisha sheria
inatumika ipasavyo,” alisema Kitillya.
Kitillya aliyasema hayo
wakati akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kumalizika
kwa sherehe za Mahafali ya Tano ya Chuo cha Kodi, kilichopo jijini Dar
es Salaam, ambapo wahitimu walikuwa ni 435 miongoni wakiwamo wanawake
137 sawa na asilimia 31.
Awali katika mahafali hayo Mwenyekiti
wa Baraza la chuo hicho, Profesa Palamagamba Kabudi akitoa hotuba yake
alisema katika kuhakikisha wanatoa huduma kwa wadau wote wa mfumo wa
kodi udahili wa wanafunzi umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.
Alisema hadi sasa chuo kimeweza kutoa jumla ya wahitimu 1,780 tangu
mwaka 2007 kiliposajiliwa. “Chuo kimeweza kuingiza mapato ya
Sh3,333,043,499.44 kwa kipindi cha miaka minne, chuo kimejiwekea mpango
wake ambao unaanza kutekelezwa katika mwaka ujao wa fedha’’ alisema.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya aliyekuwa mgeni
rasmi katika mahafali hayo, katika hotuba yake aliwapongeza wahitimu hao
na kuwataka watumie vyema ujuzi na maarifa waliyopata kwa faida ya
taifa, ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa kodi na
kuwasaidia walipakodi watimize wajibu wao wa kulipa kodi kwa
hiari.(Mwananchi)
No comments:
Post a Comment