tuwasiliane

Tuesday, January 1, 2013

KIKOSI STARS KUIKUSANYIA MAKALI MOROCCO CHATAJWA, SAMATTA, ULI NA WALIOTIMULIWA AZAM NDANI Aggrey Morris

KOCHA Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ametaja wachezaji 22 watakaoingia kambini Januari 6 mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi za kirafiki ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mechi ya mashindano dhidi ya Morocco itakayochezwa Machi mwaka huu.
 
 
Katika kikosi hicho, Kocha Mdenmark, Kim Poulsen ameendelea kuwaita wachezaji waliosimaishwa na klabu yao, Azam FC kwa tuhuma na kuhujumu timu, mabeki Erasto Nyoni na Aggrey Morris.
 
Kwa mujibu wa Kocha Kim, wachezaji wote wanatakiwa kuripoti kambini katika hoteli ya Tansoma saa 11.30 jioni tayari kwa mazoezi yatakayoanza Januari 7 mwaka huu.
 
Wachezaji walioitwa ni makipa Juma Kaseja kutoka Simba ambaye pia ndiye nahodha wa Stars, Aishi Manula na Mwadini Ally wote kutoka Azam. Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga) na Shomari Kapombe (Simba).
Viungo ni Salum Abubakar (Azam), Athuman Idd (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Frank Domayo (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar).
Washambuliaji ni John Bocco (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Mrisho Ngasa (Simba), Simon Msuva (Yanga), na Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
 
Kuhusu kuripoti, kuna kirendawili kigumu juu ya wachezaji wa Yanga, ambao wapo ziarani nchini Uturuki na watarejea kuanzia Janauri 11, mwaka huu.
Mbali ya Kim, benchi la ufundi la Taifa Stars linaundwa na Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso (Meneja), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda (Mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
 
Wakati huo huo: Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limemteua Ofisa wake, Leslie Liunda wa Tanzania kwenda Ethiopia kukagua viwanja na hoteli ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa utaratibu wa utoaji leseni kwa klabu zitakazoziwezesha kushiriki michuano inayoandaliwa na Shirikisho hilo.
 
Ofisa huyo atawasili nchini Ethiopia kesho (Januari 2 mwaka huu) ambapo anatarajiwa kukamilisha kazi hiyo Januari 6 mwakani na baadaye kupeleka ripoti yake CAF.
Utekelezaji wa kazi yake hiyo nchini Ethiopia utahusisha wadau mbalimbali ikiwemo Shirikisho la Soka Ethiopia (EFF), Wizara ya Michezo ya nchi hiyo, viongozi wa klabu na mameneja wa viwanja husika.

No comments:

Post a Comment