MSHAMBULIAJI
wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi ameongeza mkataba wa miaka miwili
kuendelea kuichezea Simba SC ya Dar es Salaam, baada ya kusaini jana usiku
katika hoteli ya Sheraton mjini hapa.
Okwi
alisaini mbele ya Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage ambaye
ameongozana na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans
Poppe.
Baada ya
kusaini, Okwi alisema; “Nimefurahi kuongeza mkataba na klabu yangu na ninaahidi
kuendelea kuitumikia kwa nguvu zangu zote,”alisema Okwi.
Kwa upande
wake, Hans Poppe alisema kwamba anaamini kusaini na Okwi sasa kutawakata
vilimilimi wapinzani wao, ambao walikuwa wanamuwania mchezaji huyo.
“Sisi
tunajua yote yaliyokuwa yakiendelea kwenye Challenge, tunajua wapinzani wetu walimfuata
Okwi huku, lakini huyu mchezaji ana mapenzi yeye mwenyewe na Simba SC,”alisema
Hans Poppe.
Okwi
aliyezaliwa Desemba 25, mwaka 1992 mjini hapa, alisajiliwa na Simba SC mwaka
2009 akitokea SC Villa ya hapa, baada
ya klabu hiyo kumkosa mshambuliaji mwingine Mganda, Brian Umony aliyewahiwa na
SuperSport United ya Afrika Kusini.
Tangu msimu
uliopita, Okwi amekuwa akihusishwa na mpango wa kuhamia Yanga au Azam na akiwa
kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker
Challenge iliyoanza Novemba 24 na inafikia tamati kesho, ziliibuka habari za
klabu hizo kumfuata kumsainisha mjini hapa.
Okwi jana
alifunga bao moja kati ya matatu ya Uganda kwenye Uwanja wa Mandela, Namboole
mjini hapa, yaliyozima ndoto za Tanzania Bara kurejea nyumbani na Kombe la
Challenge.
Kwa matokeo
hayo, Uganda itamenyana na majirani zao na wapinzani wao wakubwa, Kenya katika
fainali Jumamosi, ambao katika mchezo wa kwanza waliitoa kwa mikwaju ya penalti
4-2 Zanzibar, kufuatia sare ya jumla ya 2-2 ndani ya dakika 120.
Zanzibar na
Bara zitamenyana katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu siku hiyo hiyo ya
Jumamosi kwenye Uwanja wa Namboole.
Hadi
mapumziko, Uganda walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na Emmanuel
Okwi dakika ya 11, baada ta kuuwahi mpira mrefu uliopigwa na kipa wake, Hamza
Muwonge na kufumua shuti kali la umbali wa mita 19, ambalo lilimshinda kipa
Juma Kaseja.
Baada ya bao
hilo, Okwi aliumia na kutoka nje dakika ya 36 nafasi yake ikichukuliwa na
Hamisi Kiiza.
Uganda ndio
waliouanza mchezo huo kwa kasi na kulitia misukosuko lango la Stars kwa
takriban dakika 10 mfululizo, lakini baada ya hapo timu hizo zikaanza
kushambuliana kwa zamu.
Timu zote
zilikuwa zikishambulia kutokea pembeni, lakini Uganda ndio walioonekana kuzalisha
mashambulizi ya hatari zaidi.
Kipa na
Nahodha wa Stars, Juma Kaseja alitoka uwanjani baada ya dakika 45 za kipindi
cha kwanza akilaumiana na mabeki wake kwa kufungwa bao la kutanguliwa.
Kipindi cha
pili, Waganda walirudi na moto wao tena na kufanikiwa na kupata bao la pili
dakika ya 51, safari hii Robert Ssentongo akimtungua Kaseja, baada ya mabeki wa
Stars kudhani ameotea.
Pamoja na
kufungwa bao la pili, Stars waliendelea kucheza kwa juhudi, ingawa Waganda
waliendelea kutawala mchezo.
Mpira
uliotemwa na Juma Kaseja kufuatia shuti la Moses Oloya, ulimkuta Ssentongo
dakika ya 71 akaukwamisha nyavuni na kuipatia The Cranes bao la tatu. Kutoka
hapo, hali ilikuwa mbaya kwa Stars.
Zikiwa
zimesalia dakika tano mchezo kumalizika, taa za Uwanja wa Mandela zilizimika,
lakini baada ya jitihada za pamoja za FUFA, CECAFA na uongozi wa Uwanja,
ziliwaka baada ya dakika saba na mchezo kuendelea hadi filimbi ya mwisho.
Anasaini |
Anasaini |
Anaweka dole gumba HABARI KWA MSAADA WA BIN ZUBERY |
No comments:
Post a Comment