John Terry, baada ya kuamua kwamba hana nia ya kukata
rufaa kwa kutumia lugha ya ubaguzi dhidi ya Anton Ferdinand, na kupigwa
marufuku asicheze mechi nne na vile vile kutozwa faini ya pauni
220,000, ameomba msamaha.
Nahodha huyo wa Chelsea, atazikosa mechi nne katika ratiba ya ligi kuu ya Premier."Nataka kuomba radhi kwa lugha niliyoitumia katika mchezo huo."
Tume huru ya chama cha soka cha England, FA, ambayo ilikuwa ikichunguza madai hayo, iliamua Terry alifanya kosa la kutumia lugha ya ubaguzi wa rangi dhidi ya mlinzi wa klabu ya QPR, Anton Ferdinand, katika mechi iliyochezwa uwanja wa barabara ya Loftus, tarehe 23 Oktoba, mwaka 2011.
Terry ameadhibiwa na klabu ya Chelsea.
Hata hivyo, hatua hizo za adhabu zimehifadhiwa kama siri na klabu ya Chelsea.
Katika taarifa, klabu kimeelezea: "John Terry amefanya uamuzi unaofaa wa kuamua kutokata rufaa kuhusiana na uamuzi wa FA.
"Chelsea pia inatambua, na kuunga mkono hatua hiyo ya John kuomba radhi kikamilifu kwa lugha aliyoitumia. Klabu kinaamini lugha kama hiyo kamwe haikubaliki, na ilikuwa ni kinyume na matazamio ya mchezaji mwenye hadhi na viwango vya John kama mchezaji wa Chelsea."
Wakati huohuo, mchezaji mwenzake katika timu ya Chelsea, Ashley Cole, ametozwa faini ya pauni 90,000 kwa kuandika maneno yasiyofaa katika mtandao wa kijamii wa Twitter, katika kutofurahishwa na hatua ya chama cha FA, kuhusiana na kesi ya ubaguzi wa rangi dhidi ya Terry.
Mchezaji huyo wa Chelsea na vile vile timu ya taifa ya England, na mwenye umri wa miaka 31, alikiri kosa ambalo limetajwa na FA, la kuandika maneno yasiyofaa, na kuuletea sifa mbaya mchezo wa soka.
Cole, mara baada ya kuandika maneno hayo, aliyafuta, na kuomba msamaha.
Aliepuka adhabu ya kukatazwa kutoshiriki katika mechi, kwa kuomba msamaha, moja kwa moja kwa mwenyekiti wa chama cha FA, David Bernstein.
"Alionyesha kwa dhati kujuta hayo," alieleza Bernstein.
No comments:
Post a Comment