KLABU ya soka ya Simba inapenda kutoa taarifa zifuatazo kwenu siku ya leo.
1. Kuhusu Boban na Nyoso
Wachezaji
wawili wa Simba, Haruna Moshi Shaaban (Boban) na Juma Said Halfan
(Nyoso), wamesimamishwa kuitumikia timu ya wakubwa (senior) kwa sababu
na nyakati tofauti.
Moshi amesimamishwa kuichezea timu ya wakubwa
kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu na kutokuwa na heshima kwa
mwajiri (timu). Klabu imempa Haruna muda wa siku 21 kutoa maelezo kuhusu
makosa yake na iwapo atashindwa kutoa maelezo ya kuridhisha, klabu
inaweza kumchukulia hatua zaidi.
Katika kipindi hicho (siku 21
kuanzia jana), Boban atapokea nusu ya mshahara wake wa kila mwezi na
hatapata marupurupu yoyote yanayohusiana na timu ya wakubwa.
Kwa
upande wa Nyoso, uongozi umemwagiza afanye mazoezi na kikosi cha timu ya
pili (Simba B) hadi hapo atakapoimarisha kiwango chake cha uchezaji.
Hatua hii imetokana na ripoti ya benchi
la ufundi iliyoonyesha kwamba mchezaji huyo amekuwa akifanya makosa
mengi ya kiuchezaji yanayoigharimu na ingawa amekuwa akipewa maelekezo
na walimu, bado amekuwa akirudia makosa yaleyale.
Kutokana na
hilo, Nyoso atafanya mazoezi na wachezaji wa kikosi cha pili hadi walimu
watakaporidhika kwamba amejirekebisha na yuko tayari kutumikia kikosi
cha wakubwa.
Katika muda wake wote huo akifanya mazoezi na timu
B, Nyoso atakuwa akipata mshahara wake wa kila mwezi kama kawaida na pia
atapata marupurupu wanayopata wachezaji wa Simba B.
Emmanuel Okwi
Klabu
ya Simba inaeleza kusikitishwa kwake na taarifa za vyombo vya habari
vyenye lengo la kuuza magazeti pasipo kujali athari za habari zenyewe.
Kwa
mfano, habari ya kwenye gazeti la CHAMPIONI la leo ina kichwa cha
habari KATIBU MKUU AMFUKUZA OKWI SIMBA. Hata hivyo, kilichoandikwa ndani
ya habari yenyewe kinamnukuu aliyewahi kuwa Katibu Mkuu kwenye miaka ya
nyuma.
Gazeti hilo linafahamu kabisa kwamba Simba ina Katibu
Mkuu mmoja tu kwa sasa na anaitwa Evodius Mtawala. Simba haijawahi kuwa
na makatibu wakuu wawili kwa wakati mmoja.
CHAMPIONI linafahamu
ukweli huu lakini kwa sababu inazozijua lenyewe, imeamua kuandika habari
hiyo na kuweka kichwa cha habari cha namna hiyo pasipo kujali athari
zake kwa wanachama wa Simba, Katibu Mkuu aliyepo madarakani kwa sasa na
weledi wa fani ya uandishi wa habari
Kilichoandikwa kwenye habari
hiyo ya CHAMPIONI ni maoni binafsi ya mwanachama wa Simba na kwa mujibu
wa Katiba ya Tanzania, kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake kuhusiana
na jambo lolote ali mradi halivunji sheria za nchi.
Simba SC
inarudia wito wake wa kuvitaka vyombo kubaki kwenye misingi ya kitaaluma
na kuacha kuandika habari zilizotiwa chumvi na kuleta mitafuruku isiyo
na sababu yoyote.
Kikosi
Simba inaendelea vizuri na
mazoezi visiwani Zanzibar kujiandaa na mechi dhidi ya Azam itakayopigwa
katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi hii.
Hata
hivyo, mchezaji Salim Kinje ameruhusiwa kuondoka kambini Zanzibar leo
kutokana na kupata msiba wa baba yake mkubwa uliotokea Dar jana.
Uongozi, kwa namna ya kipekee kabisa, unatoa salamu za pole kwa familia ya Kinje kutokana na msiba huu.
Boniface Wambura
Kwa
niaba yangu binafsi na klabu ya Simba, napenda kumpongeza Ofisa Habari
wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, kwa
kuteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuwa miongoni mwa
wasimamizi wa shirikisho hilo katika michuano ya Wanawake
itakayofanyika nchini Guinea ya Ikweta (Equatorial Guinea).
Wambura
ndiye Mtanzania pekee aliyeteuliwa na CAF kutumika kwenye michuano hiyo
na jambo hilo ni la faraja kwa tasnia ya habari nchini ambako Wambura
ametokea.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC
No comments:
Post a Comment