MAKATO
ya ajabu ajabu, yasiyo na msingi na mengine mengi yanayofanana, ambayo
yanabadilishwa-badilishwa majina tu licha ya kubeba maana moja,
yameendelea kuzikamua hadi tone la mwisho klabu za ligi kuu katika
kampeni "nzito" ya kuhakikisha haziendelei.
Katika mechi ya Ligi Kuu
ya Vodacom baina ya Simba na Kagera Sugar iliyochezwa Oktoba 17 kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya mabao
2-2, Sh. milioni 58.5 zilipatikana lakini kila klabu iliambulia mgawo
kiduchu wa Sh. milioni 11.1 tu.
Hali hiyo iliendelea pia katika mechi
ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting iliyochezwa Jumamosi Oktoba 20 kwenye
Uwanja wa Taifa na kumalizika kwa wenyeji kushinda 3-2.
Licha ya mechi hiyo kuingiza Sh. milioni 47.6, Yanga na Shootings kila moja iliambulia mgawo kiduchu wa Sh.
milioni 8.4.
Ni makato makubwa yanayozua maswali tele ambayo majibu yake hayajawahi kutolewa.
Kwa kutumia mfano wa mechi ya Simba dhidi ya Kagera Sugar, makato halisi yalikuwa kama ifuatavyo:
1. Maandalizi ya uwanja (pitch preparation) Sh. 400,000
2. Uwanja Sh. 3,671,261.85
3. Usafi na ulinzi wa uwanja Sh. 2,350,000
4. Ulinzi wa mechi Sh. 3,500,000
5. Gharama za mchezo Sh. 3,671,261.85
6. Umeme Sh. 300,000
7. Wachina (stadium technical support) Sh. 2,000,000
8. Tiketi ni Sh. 3,183,890.
9. Posho ya msimamizi wa kituo Sh. 120,000
10. Kamishna wa mechi Sh. 250,000
11. Waamuzi Sh. 440,000
12. Mwamuzi wa akiba Sh. 70,000
13. Mtathimini wa waamuzi Sh. 254,000
14. Kamati ya Ligi Sh. 3,671,261.85
15. Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) Sh. 2,202,757.11
16. Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Sh. 1,468,504.74.
17. Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni Sh. 8,924,491.53.
Kwa
mchanganuo huo inamaanisha kwamba zaidi ya Sh. milioni 36 zilimezwa
katika makato wakati klabu ziliambulia jumla ya Sh. milioni 22.
Vilio
vimekuwa vikubwa sasa kwa sababu ni makato mengi mno yanayoua timu zetu
changa ambazo zinahitaji sapoti ya serikali, ambayo badala yake imekuwa
ikizikamua.
Miongoni mwa makato yanayochefua ni ya "Uwanja",
"Maandalizi ya Uwanja", "Usafi wa Uwanja na Ulinzi" na "Ulinzi wa
mechi". Ni kwa vipi unaweza kumshawishi mtu kwamba hivyo ni vitu vinne
tofauti?
Miongoni mwa maswali magumu ambayo hayajatolewa majibu ni haya:
UWANJA
Makato
ya "Uwanja" peke yake, yanathibitisha kwamba uwanja huo unakodishwa,
hivyo ili kuutumia ni lazima ulipie. Ndio maana Simba na Kagera Sugar
wakatozwa Sh. milioni 3.6. Je, klabu zinaruhusiwa kuukodi kwa kulipa
mapema kiasi hicho cha pesa na kisha waone wenyewe kama watahitaji
kulipia umeme, kama watahitaji sapoti ya kiufundi kutoka kwa Wachina?
MAANDALIZI
YA UWANJA
Malipo ya "Uwanja" yanatumika kufanya kazi gani ikiwa pia kuna malipo ya "Maandalizi ya Uwanja" na "Gharama za Mchezo"?
Tofauti
ya malipo haya iko wapi? Je makato ya 'Usafi wa Uwanja na Ulinzi" siyo
"Maandalizi ya Uwanja"? Kwani mtu anaposema maandalizi ya uwanja huwa
anamaanisha nini?
USAFI WA UWANJA NA ULINZI
Licha ya kuwapo
kwa makato ya "Maandalizi ya Uwanja" pia kuna makato haya ya "Usafi wa
Uwanja na Ulinzi". Je, wanapofanya usafi uwanjani hayo siyo maandalizi
ya uwanja? Na kama usafi ni maandalizi ya uwanja, kwanini ni makato
tofauti? Na "ulinzi' huu ni upi ambao kwa pamoja na usafi unagharimu
jumla ya Sh. milioni Sh. 2,350,000 ikiwa vyoo ni vichafu na unaweza
ukazimia ukipita nje tu, acha kuingia ndani?
ULINZI WA MECHI
Licha
ya kwamba makato ya ulinzi yameshakatwa katika kategori iliyopita ya
"Usafi na Ulinzi", pia kuna makato mengine tofauti ya "Ulinzi" pekee
ambayo yanagharimu Sh. milioni 3.5. Kama uwanja
unalindwa na askari polisi ambao wanalipwa mishahara na serikali
iliyowaajiri kwa ajili ya kulinda nchi, fedha hizi Sh. milioni 3.5
zinakwenda wapi?
GHARAMA ZA MCHEZO
Makato ya zilizopewa jina
la "gharama za mchezo" katika mechi ya Simba dhidi ya Kagera Sugar
zilikuwa Sh. milioni 3.67. Je, gharama za mchezo hazipaswi kujumuisha
malipo ya waamuzi, ulinzi wa mechi, usafi na maandalizi ya uwanja?
Kwanini haya ni makato tofauti?
UMEME
Kwa mfano umeme hulipiwa
Sh. 300,000 katika takriban kila mechi ilhali mechi karibu zote
huchezwa mchana? Fedha hizi zinazokatwa pengi mara tatu (Sh. 900,000)
katika siku 8 zinaenda kulipia umeme upi? Wa Tanesco au wa jenereta? Ni
kweli umeme wa kila saa 2 kwenye uwanja ule ni Sh. 300,000? Au klabu
zinakamuliwa ili kulipia umeme wa hata siku ambazo hawautumii?
WACHINA
Wachina
hawa wapo kutoa sapoti ya kiufundi. Je, anayepaswa kuwalipa ni mmiliki
wa uwanja ama anayeukodi? Hii sapoti ya kiufundi
inayogharimu Sh. milioni 2 mara tatu (Sh. milioni 6) ndani ya siku 8 ni
ipi? Wanatoa sapoti gani ya kiufundi katika mechi hizi zinazochezwa
mchana kweupe? Ikiwa mechi zenyewe hazirushwi na kituo chochote cha TV
na hata wakirusha hawatumii chumba (control room) cha uwanja wanatumia
magari yao ya 'van', ni sapoti gani wanayotoa Wachina hawa?
Makato
ya Wachina yanashangaza, kwani wao ndiyo waliojenga uwanja kwa pesa ya
msaada wa nchi yao na pia Serikali ya Tanzania. Sasa cha kujiuliza ni
kwamba uwanja ule bado uko mikononi mwao?
Je, walipomaliza kujenga uwanja hawakuukabidhi kwa Watanzania na badala yake wakaingia ubia kuumiliki?
Ina
maana Uwanja wa Taifa unamilikiwa na Wachina upande mmoja na Serikali
upande mwingine ndiyo maana kila mmoja anakuwa na makato yake?
VAT
Makato
ya ongezeko la thamani (VAT) katika mechi hii ya Simba dhidi ya Kagera
Sugar yalikuwa Sh.8,924,491.53. Kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria za kodi
hapa. Ikiwa pia kuna
makato ya umeme, ambapo kwenye umeme pia huwa kuna VAT, je, ni sahihi
kulipa VAT mara mbili katika 'bidhaa' (mechi) moja?
DRFA
Lakini
pia hivi makato ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam DRFA
ni ya nini na yanakwenda kufanyia kazi gani ikiwa kwa sasa vyama vya
soka vya wilaya za Dar es Salaam (KIFA - Kinondoni, TEFA - Temeke na
IDFA - Ilala) vyote vimeshapewa hadhi ya mikoa na vinaendesha ligi zao.
Mratibu
wa Mtibwa Sugar, Jamal Bayser alisema makato hayo yanawaumiza na
kuwakwaza kiuchumi, hivyo akazitaka klabu kuungana ili kulipatia
ufumbuzi suala hilo ambalo limekuwa tatizo kubwa kwa maendeleo ya klabu
za soka nchini.
Naye meneja wa Azam, Patrick Kahemele anazigeukia
klabu kuwa zenyewe ndizo zinapaswa kujilaumu kwa kuipa madaraka makubwa
TFF katika kupanga gharama za tiketi, kiingilio na makato mengine ya
gharama za mechi husika, hali ambayo mwishowe huwaacha wakiambulia fedha
kidogo mno kutokana na mapato ya
milangoni.
“Haya yote yanatokea kwa sababu mwanzo wetu haukuwa
mzuri. Klabu hazina umoja. Kama tungeungana katika hili, kusingekuwa na
malalamiko,” alisema Kahemele na anaongeza
“Vitabu vya tiketi za
uwanjani viko TFF na klabu hazioneshwi, kuna gharama za waamuzi, ulinzi,
gharama za mchezo, maandalizi ya uwanja, gharama za mchezo, pesa ya
Kamati ya Ligi. Katika hali kama hii tunategemea klabu itanufaika na
kiingilio cha mechi."
Mmoja wa wamiliki wa klabu ya African Lyon,
Rahim Kangezi naye anasema wamekuwa wakisikitishwa na hali ya makato
inayofanywa na TFF na serikali dhidi ya klabu za Ligi Kuu.
Afisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga anasema klabu yao pia imekuwa ikiathiriwa na makato makubwa.
Katika
mkutano wake na waandishi wa habari hivi karibuni, Rais wa TFF, Leodgar
Tenga alisema kuwa makato yote katika kila mechi yanafuata sheria na
taratibu zilizopo.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema asilimia 60 ya makato yote
inakwenda serikalini na kwamba pia wanalazimika kutoa fedha Sh. 200,000 kwa ajili ya mafuta ya magari ya polisi.
Simba
na Yanga ziliwahi kutishia kutocheza tena kwenye Uwanja wa Taifa
kuepuka makato makubwa misimu kadhaa iliyopita na Serikali iliwapoza kwa
kuahidi kushughulikia suala hilo.
Hata hivyo, inaonekana hakuna
juhudi za kulishughulikia suala hilo hivi karibuni, licha ya Katibu Mkuu
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Sethi Kamuhanda,
kuiambia NIPASHE hivi karibuni kwamba wanaweza kukaa chini kuliongelea
jambo hilo.
Lakini pamoja na hayo, kinachoonekana hapa bila klabu kuunganisha nguvu na kupinga hili hakuna chochote kitakachofanyika.
Source: Gazeti la Nipashe
No comments:
Post a Comment