tuwasiliane

Thursday, October 18, 2012

Peter Rufai akimbizwa hospitali

Aliyekuwa kipa wa zamani wa timu ya taifa ya Nigeria, Peter Rufai, Jumatatu usiku alikimbizwa hospitali baada ya kuzimia.
Rufai, mwenye umri wa miaka 49, na aliyeiwakilisha nchi yake katika fainali za Kombe la Dunia miaka ya 1994 na 1998, alikimbizwa hadi hospitali ya Toki, mjini Lagos, mara tu baada ya kupoteza fahamu.

Ndugu yake, Bruce, alisema alipozimia, ilionekana alikuwa na matatizo ya kupumua, na wakaamua ni vyema kumkimbiza hospitali.

"Lilikuwa ni jambo la kushtua mno alipoanguka na kuzimia, na kupoteza fahamu kabisa," Bruce aliielezea BBC.

"Yote hayo yalifanyika kwa haraka, na tulishuhudia mtu mwenye nguvu na mwenye akili timamu ghafula akianguka chini."

Tangu kufikishwa hospitali, Bruce ameelezea kwamba ndugu yake ni afadhali sasa ikilinganishwa na namna alivyokuwa alipopelekwa hospitali.

Alieleza: "Baada ya saa chache, alipata fahamu, na akaweza kuwatambua baadhi ya watu waliomtembelea hospitalini, na kwa hiyo nadhani yumo katika hali nzuri kuliko alivyokuwa Jumanne asubuhi."

"Madaktari wameshindwa kugundua maradhi yake, na tuna hisia kwamba chanzo ni hali ambayo imekuwepo ya maombolezi katika familia.

"Inaelekea alipata mshituko kufuatia kifo cha mama yetu, na hatujui atalazwa hospitalini kwa muda gani."

Mamake Peter Rufai, Christiana Rufai, alifariki wiki iliyopita, akiwa na umri wa miaka 78.

Rufai alikuwa ni kipa bora zaidi wa timu ya Nigeria ilipotwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika nchini Tunisia, mwaka 1994, na walipofuzu kwa mara ya kwanza kushiriki katika fainali za Kombe la Dunia.

Yeye ni kati ya watu walioweza kuwa walinda lango bora zaidi barani Afrika, na akijulikana kwa jina la utani kama 'Dodo Manyana'.

Aliwahi kucheza kama mchezaji wa kulipwa katika mataifa ya Benin, Ubelgiji, Uholanzi, Uhispania na Ureno.

Tangu alipoacha kucheza soka, amekuwa akihusika na timu ya taifa ya Olimpiki, na vile vile chuo chake cha mafunzo ya soka mjini Lagos.

No comments:

Post a Comment