tuwasiliane

Thursday, October 18, 2012

Matajiri wa Simba wamfanyia balaa Okwi

KWA dau Emmanuel Okwi alilopandiwa na matajiri wa Simba kwenye mkataba mpya, beki ghali wa Yanga, Mbuyu Twite haoni ndani. Mshahara na dau la usajili wa Twite kwa mwaka havizidi Sh 93.5 milioni.

Simba imepandisha thamani ya straika wake, Okwi ambaye atavuna Sh. 134 milioni kwa mwaka kama atasaini mkataba mpya wa mwaka mmoja dakika yoyote kuanzia sasa.

Hiyo ina maana kuwa licha ya kuzidiwa kidogo mshahara na Mzambia Felix Sunzu anayelipwa Dola 3,500 (Sh 5.5 milioni) lakini Okwi akiweka pamoja dau jipya la usajili pamoja mshahara mpya kwa mwaka mzima ataweka benki Sh 134 milioni ambazo ukiongeza Sh. 2 milioni hapo unapata mshahara wa wachezaji wote wa Simba wa kigeni kwa mwaka Sh 136 milioni.

Okwi alitarajiwa kurejea nchini jana Jumatatu baada ya kumalizika kwa mechi ya Uganda na Zambia ya kuwania kufuzu fainali za Afrika ambako Uganda ya Okwi ilitolewa kwa penalti 9-8.

Katika mkataba wa Okwi unaomalizika mwezi ujao alikuwa akilipwa Dola 800 (Sh 1.2 milioni) kwa mwezi lakini masharti yamebadilika kwenye mkataba mpya ambao matajiri wa Simba wameridhia kumpa kila anachotaka.

Habari za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba Okwi amewapa viongozi masharti mawili. Mosi, wampe Dola 50,000 (Sh. 77.7 milioni) za usajili pamoja na kupandisha mshahara wake kufikia Dola 3,000 (Sh.4.6 milioni).

Viongozi hao wameridhia kumpa mshahara wa Dola 3,000 ambazo thamani yake kwa mwaka mzima ni Sh. 55.8 milioni ukiongezea na dau la usajili la Dola 50,000 ambazo ni Sh 77.7 milioni za Tanzania.

Okwi alifanya mazungumzo ya kina na mabosi wake wiki iliyopita na kuwaachia changamoto hiyo ambayo walimjibu baadaye kwamba haina matatizo watampa.

Mchezaji huyo amekuwa tegemeo kwenye kikosi cha kwanza cha Simba lakini mkataba wake unaomalizika unaonyesha kuwa ndiye mchezaji aliyekuwa akilipwa fedha ndogo zaidi ya wote wa kigeni wa Simba na Yanga.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa CHANZO CHETU ndani ya Simba, umebaini kwamba straika Sunzu analipwa Dola 3,500 (Sh 5.5 milioni) kwa mwezi akifuatiwa na beki Komanbilli Keita wa Mali na mshambuliaji Daniel Akuffo wa Ghana wote wanalipwa Dola 1,000 kwa mwezi ambazo ni sawa na Sh 1.6 milioni.

Beki Mkenya, Paschal Ochieng analipwa Sh 1.2 milioni kwa mwezi sawa na straika mpambanaji Okwi anayelipwa Dola 800 ambazo ni sawa na Sh.mil.1.2.

Kwa upande wa Yanga, Mkongomani mwenye uraia wa Rwanda, Mbuyu Twite anaongoza orodha kwa kulipwa anapata Dola 2,500 sawa na Sh.3.8 milioni akifuatiwa na Mnyarwanda Haruna Niyonzima na Yaw Berko wa Ghana wanaokinga Dola 1,500 kila mmoja ambazo ni sawa na Sh 2.4 milioni kwa mwezi.

Straika wa Burundi, Didier Kavumbagu analipwa Dola 1,200 sawa na Sh 1.9 milioni huku Kiiza wa Uganda akishikilia nafasi ya mwisho kwa wageni wa Yanga kwa kulipwa Dola 1,000 ambazo ni Sh 1.6 milioni.

No comments:

Post a Comment