Friday, October 26, 2012
HARUNA MOSHI: MCHEZAJI MWENYE KIPAJI, MTUKUTU ANAYEHARIBIWA NA MASHABIKI - SIMBA ILICHELEWA KUMSIMAMISHA
Siku ya juzi klabu ya Simba ambao ndio mabingwa watetezi wa ligi kuu ya Tanzania bara walitoa taarifa ya kuwasimamisha wachezaji wake wawili wa kikosi cha kwanza Haruna Moshi Shabaan aka Boban na Juma Nyosso kutoka na sababu mbili tofauti.
Juma Nyosso alisimamishwa kuichezea klabu ya wakubwa ya Simba na kupelekwa kufanya mazoezi na timu ya pili ya klabu hiyo ili aweze kurudisha kiwango chake ambacho kimeporomoka sana msimu huu. Huku Haruna Moshi Boban akisimamishwa kuichezea timu hiyo kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu vilivyokithiri.
Masuala ya vitendo vya ukosefu wa nidhamu kwa Boban sio mageni kabisa, pamoja na kipaji kikubwa alichonancho cha soka lakini Boban ni mmoja ya wachezaji wenye nidhamu mbovu katika soka la kizazi hiki.
Boban kwa kipindi cha muda mrefu amekuwa akifanya matukio ya ajabu ndani na nje ya uwanja, na anapoadhibiwa baadhi ya wadau na mashabiki wa soka wanamtetea na kudai anaonewa.
Pamoja na sifa ya utovu wa nidhamu baadhi ya makocha ambao tayari wameshafanya kazi na mchezaji huyu kipenzi cha mashabiki hasa wa klabu yake ya Simba, wanasema kwamba Boban pia ni mchezaji mvivu mno, na hana utaratibu mzuri wa kuishi kama mchezaji wa soka la kisasa, na ndio maana pamoja na kipaji kikubwa alichonacho imeshindikana kwa mchezaji huyu kucheza soka nje ya nchi kwa mafanikio.
Kwa taarifa za uhakika nilizonazo, zipo sababu kadhaa zisizopungua nne ambazo ndizo zimepelekea Boban kusimamishwa Simba.
Wakati Simba ikiwa inajiandaa na mchezo dhidi ya Mgambo JKT, Haruna akidai anaumwa hivyo hatoweza kwenda timu jijini Tanga. Uongozi ukampa ruhusa, lakini wakati timu ikiwa tayari Tanga, Boban akaonekana maeneo ya uwanja wa Muhimbili akicheza ndondo. Kama hiyo haitoshi usiku wake akaonekana katika moja ya kumbi za starehe akijirusha - kwa bahati nzuri hapo katika kiwanja cha kujirusha alikuwepo mmoja wa viongozi wa Simba kutoka kamati ya usajili ambaye alimuona Boban na kuupeleka uongozi wa juu taarifa juu ya mchezaji huyo.
Boban akaitwa na uongozi na kuhojiwa juu ya suala hilo, na baada ya hapo mchezaji huyo akafikia hatua ya kumpigia simu kiongozi aliyemchongea kwa uongozi wa klabu na kumtukana matusi makubwa ya nguoni.
Pia Boban amekuwa akilalamikiwa kufanya mambo anavyojisikia ndani ya Simba, kwanza taarifa kutoka benchi la ufundi mchezaji huyo ni mvivu wa mazoezi na anacheza anavyojisikia yeye, pili hana utaratibu mzuri, kwa mfano timu inapocheza Dar es Salaam wamejipangia utaratibu wa kukutana klabuni na kuondoka kwa pamoja kwenye basi rasmi la timu, lakini Haruna amekuwa akipingana na utaratibu huo na kuacha kupanda basi hilo kisha huenda uwanjani na gari lake binafsi.
Jambo lingine timu yenye udhamini kama Simba imejiwekea sare maalum za kuvaa staffs wa timu hiyo wakati wa kabla ya mechi, kwenye mechi na baada ya mechi, lakini Haruna amekuwa akijivalia vyovyote anavyojisikia hivyo kuharibu utaratibu ambao timu imejiwekea.
Pamoja kuendelea na matendo yake ya utovu wa nidhamu huku akionywa mara kwa mara Boban aliendelea kukaidi na hatimaye juzi uongozi wa Simba ukaamua kumsimamisha mchezaji huyo a.k.a 'kichwa haambiliki'
Boban ni mchezaji tegemeo Simba hivyo anapofanya mambo ya ajabu anaihathiri timu yake ambayo ilianza ligi vizuri lakini sasa mambo yameanza kwenda hovyo.
Ili mchezaji ucheze kwa kiwango kuzuri inabidi ufanye mazoezi kwa bidii, kusikiliza na kufuata unachofundishwa na mwalimu pamoja na kuwa na nidhamu nzuri na mwisho ndio kinakuja kipaji binafsi. Boban anakosa vyote hivyo anabaki na kipaji tu, kitu ambacho pekee yake hakitoshi kumkamilisha mchezaji wa soka la kisasa.
source; shaffih dauda website
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment