Friday, September 14, 2012
TFF yatoa vifaa Hospitali ya Temeke
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) litatoa vifaa vyenye thamani ya Sh7.3 milioni kwa Hospitali ya Temeke, mkoani Dar es Salaam ikiwa ni asilimia 5 ya fedha zilizopatikana kwenye mechi ya Ngao ya Jamii iliyozikutanisha Simba na Azam.
Mechi hiyo ya Ngao ya Jamii kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ilichezwa Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, uliingiza Sh 146, 640,000.
Jumla ya mashabiki 26,001 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa Simba kushinda mabao 3-2.
Kwa mujibu wa Ofisa wa Habari wa TFF, Boniface Wambura, Sekretarieti ya TFF inatarajia kukutana na uongozi wa Hospitali ya Temeke ili kujua mahitaji halisi kabla ya kufanya ununuzi wa vifaa husika.
Iwapo TFF itatekeleza ahadi hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kuitimiza baada ya miaka miwili mfululizo fedha hizo kutafunwa bila ya kuwafikia walengwa.
Mwaka juzi fedha hizo zilielekezwa kwa wahanga wa mabomu ya Gongolamboto, lakini ilikuwa kinyume kwani hazikufika kwa walengwa na mwaka jana TFF ilipanga fedha hizo za Ngao ya Jamii kupelekwa Chama cha Madaktari Wanawake (Mewata) kwa ajili ya kusaidia kampeni za kupambana na saratani ya matiti hata hivyo hawakuziwasilisha kitendo ambacho kilileta mvutano na Mewata.
TFF baada ya kubanwa na vyombo vya habari walikiri kuzitumia fedha hizo za Mewata kwenye mahitaji mengine na kuahidi kuzilipa.
Fedha ambazo ilikuwa Mewata ipate ni asilimia 15 ya mapato yaliyopatikana kwenye mechi ya Ngao ya Hisani kati ya Simba na Yanga.
Hata hivyo mmoja wa Madaktari wa Mewata, Dk Lilian aliiambia Mwananchi kuwa TFF walizipeleka fedha hizo mwezi wa sita mwaka huu.
"Tunashukuru mlitusaidia, baada ya kuzihangaikia sana mwezi wa sita mwaka huu walituletea," alisema Dk Lilian.
Mchango wa kusaidia jamii kwenye mechi ya Ngao ya Jamii kuzindua msimu uliopita kati ya Yanga na Simba ulikuwa Sh15,000,000 ambazo zilikwenda Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (Mewata) kusaidia uchunguzi wa saratani ya matiti.
Katika mchezo wa Jumanne wa Ngao ya Jamii kati ya Simba dhidi ya Azam, jumla ya Sh146, 640,000 zilipatikana, ambapo TRA walichukua asilimia 18 ya mapato hayo ambayo ni Sh22,368,813.56, asilimia 5 ya mchango wa kusaidia jamii (Hospitali ya Temeke) Sh7,332,000, uwanja Sh10,148,318.64, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Sh4,059,327.46, TFF Sh10,148,318.46 na Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) Sh5,074,159.32.
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Sh1,014,831.86, kila timu ikiambulisha Sh32,265,025.93, asilimia 10 ya gharama za mchezo Sh10,148,318.64, nauli kwa waamuzi na kamishna Sh80,000, posho ya kujikimu kwa waamuzi na kamishna 230,000, posho ya waamuzi 400,000, tiketi Sh4,495,800, maandalizi ya uwanja (pitch) Sh400,000, umeme Sh300,000, usafi na ulinzi uwanjani Sh2.350,000 na Wachina (Beijing Construction) Sh2,000.000.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment