tuwasiliane

Saturday, September 8, 2012

Simba, Azam kusaidia hospitali ya Temeke


ASILIMIA tano ya mapato yatakayopatikana katika mechi ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kati ya Simba na Azam itakayochezwa Jumanne ijayo kwenye Uwanja wa Taifa yatakwenda hospitali ya Temeke, Dar es Salaam.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema kuwa kabla ya kukabidhi fedha hizo TFF itakutana na uongozi wa hospitali ya Temeke kupanga maeneo ambayo fedha hizo zitatumika katika hospitali hiyo.

"TFF itakutana na uongozi wa hospitali ya Temeke ili kupatiwa ufafanuzi wa jinsi fedha hizo zitakavyotumika, lengo likiwa ni kutimiza kauli mbiu ya mchezo huo yaani Ngao ya Jamii,"alisema Wambura.

Alisema mechi hiyo ya uzinduzi rasmi wa msimu wa 2012/2013 itaanza saa 10:00 jioni, huku viingilio vikiwa sh 5,000 kwa viti vya rangi ya bluu na kijani, sh 10,000 viti vya rangi ya chungwa, sh 15,000 kwa viti vya VIP C na B wakati VIP A itakuwa sh 20,000.

Wakati TFF ikisema kuwa fedha zitakazopatikana kwenye mchezo huo asilimia tano zitakwenda kusaidia jamii kwa kuiwezesha Hospitali ya Temeke hadi leo bado hawajawasilisha fedha walizoahidi kuzipeleka kwenye chama cha madaktari wanawake Tanzania (MEWATA) zilizopatikana katika mechi kama hii msimu uliopita, ambapo ulizikutanisha timu pinzani Simba na Yanga.

Katika historia ya soka hapa nchini mechi hiyo ya Ngao ya jamii itakuwa ni mechi ya tano kuchezwa, pia ni mechi ya pili kukutanisha timu ambazo siyo wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.

Vilevile ni mara ya kwanza kwa timu ya Azam kunyang'anyana Ngao hiyo na Simba.

No comments:

Post a Comment