tuwasiliane

Saturday, September 8, 2012

AY autwaa UBALOZI wa Airtel!




Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel imemtangaza msanii wa kizazi kipya, Ambwene Yessaya maarufu kwa jina la AY, kuwa balozi wake mpya kwa mwaka 2012/2013 ikiwa ni utaratibu iliyojiwekea kushirikiana na wasanii kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.

Kwa mujibu wa Meneja Uhusiano wa Airtel, Jackson Mmbando, alisema wameingia makubaliano na AY kuwa Balozi wao kwa mwaka huu, lengo likiwa ni kuendelea kuwa karibu zaidi na wasanii na kufanya nao shughuli za kijamii.

Alisema AY ni msanii mahiri nchini katika muziki wa kizazi kipya, aliyejipatia heshima na kuvuta hisia za wapenda burudani wengi pale anapokuwa jukwaani.

“Kufaidisha Taifa letu kwa kuwa wasanii wetu ni mahiri zaidi na wote tunafahamu AY ni msanii mkongwe na anayejituma, hivyo tunaamini ushirikiano huu utaweza kutimiza malengo yetu ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa pamoja kuhudumia jamii kupitia miradi mbalimbali ya jamii inayoendeshwa na Airtel pamoja na kuiwakilisha Airtel kwa kuwa balozi mzuri.

“Sasa AY atakuwa ni msanii wa pili kuingia mkataba kama huu ambapo mwaka uliopita alikuwa Ali Kiba. Tulimtangaza Ali kiba kuwa Balozi wa Airtel mwaka jana.

“Ameshirikiana na Airtel kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kuitangaza Airtel kupitia matangazo ya redio, luninga na mabango lakini pia alifanikiwa kuiwakilisha nchi yetu katika wimbo wa Hands Across the World alioimba na wasanii wengine wa kimataifa akiwemo R. Kelly katika kundi la One8 kwa udhamini wa Airtel,” alisema Mmbando.

Alisema AY ni msanii mwenye umahiri wa hali ya juu anapokuwa jukwaani na amefanikiwa kufanya matamasha ya kimataifa Marekani, Uingereza, Hispania, Dubai, Burundi, Rwanda, Ethiopoa, Malysia, India, Russia, Afrika ya Kusini, Kenya na Uganda.

Kwa upande wake, AY, alisema kwa kushirikiana na Airtel atakuwa akifanya shughuli za kijamii hususani katika kuchangia ukuaji wa elimu hapa nchini.

“Pamoja na Airtel, tutashirikisha vyombo na taasisi nyingine vikiwamo vyombo mbalimbali vya habari kuweza kufanikisha yote hayo.

“Kwa kushirikiana na Airtel tutaandaa maonyesho mbalimbali ya burudani kwa ajili ya wateja na hii itatangazwa hivi karibuni.

“Kwa kuanza kama Balozi wa Airtel napenda kuwaomba na kuwahimiza Watanzania wenzangu kuweza kuchangia mradi ambao tumeshauanzisha wiki tatu zilizopita tukishirikiana na BAMVITA katika kuchangia vitabu kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalumu.

“Kampeni hii ya ushirika na BAMVITA itaendeshwa kwa muda wa miezi mitatu na Watanzania tunaweza kuchangia kwa kutuma neno vitabu kwenda namba 15626 na kwa kufanya hivyo kila sms tutakayotuma utakuwa umechangia shilingi 200 itakayoingizwa yote katika mradi huu,” alisema AY.

No comments:

Post a Comment