tuwasiliane

Tuesday, September 18, 2012

Mourinho na Mancini wasema City wataibuka washindi


Meneja wa klabu ya Real Madrid ya Uhispania, Jose Mourinho, amesema anaamini Manchester City ya England ina uwezo wa kuunyakua ubingwa wa klabu bingwa barani Ulaya hivi karibuni.

Akizungumza kabla ya pambano lao la Jumanne jioni mjini Madrid, meneja wa Manchester City, Roberton Mancini, alikubaliana na matamshi hayo ya Mourinho, akisema ni kweli wanatazamia ushindi huo hivi karibuni.

"Ikiwa unaendesha Ferrari unaweza kushinda, ikiwa ni Fiat Cinquecento, pengine haitawezekana," alisema Mancini.

Mourinho alisema: "Kutokana na muelekeo wa klabu, hivi karibuni huenda wakalipata kombe hilo kubwa."

Mourinho, ambaye zamani alikuwa ni meneja wa Chelsea, aliufananisha uwekezaji katika klabu ya City, kama alivyowekeza Roman Abramovich, mmiliki wa klabu hiyo ya Stamford Bridge.

Meneja Mourinho aliweza kuiletea Chelsea ubingwa mara mbili wa ligi kuu ya Premier, lakini akashindwa kuwawezesha kupata kombe la klabu bingwa, ambalo alilipata akiviongoza vilabu vya Porto na Inter Milan.

Hatimaye Chelsea walilipata kombe hilo msimu uliopita chini ya Roberto Di Matteo, na Mourinho ana imani City wako njiani kuupata ubingwa wa Ulaya.

Alisema: "Nadhani sio tofauti sana na Chelsea.

"Tangu Roman alipoinunua klabu, (Claudio) Ranieri alikuwa kocha wa kwanza, kisha nikaingia mimi na kupata ushindi wa kwanza wa ligi, vikombe kadha na mataji kadha.

"Carlo (Ancelotti) kisha akaja, na wakaendelea kupata ushindi, na hatimaye walilipata kombe la klabu bingwa."

No comments:

Post a Comment