
STRAIKA namba moja wa Simba, Mghana Daniel Akuffo amemtia wazimu kocha, Milovan Cirkovic ambaye ametamka kwamba akisimama na Felix Sunzu itakuwa tishio la mwaka.
Akuffo amecheza mechi tatu za kirafiki tangu ajiunge na Wekundu hao na amepachika bao moja moja kila mechi huku akichezeshwa dakika 50 mpaka 60 kila mechi.
Kocha Milovan aliiambia Mwanaspoti jana Jumatatu kuwa straika huyo ameonyesha kiwango kizuri mpaka sasa na ana imani atakuwa imara zaidi akiungana na Sunzu na Okwi.
"Ameonyesha kiwango kizuri sana na anajituma sana ndio maana kila mechi anafunga, ni straika mzuri ambaye nadhani atafanya kazi kubwa sana kwa Simba msimu huu.
"Akiungana na Felix Sunzu watafunga mabao mengi zaidi, kwa kuwa watakuwa na muunganiko mzuri zaidi ambao utatengeneza mabao mengi, lengo letu msimu huu ni kufanya vizuri kadri inavyowezekana.
"Kufunga mabao mengi pamoja na kutetea ubingwa wetu mapema, hizi mechi za kirafiki zimetoa mwanya wa mimi kujua kila mchezaji ana kitu gani cha tofauti ndio maana umeona nilikuwa nawachanganyachanganya sana, kujua nani ana kitu gani na anaweza kukitumiaje.
"Mimi suala la timu kuruhusu mabao halinistui sana kwa kuwa ilikuwa ni sehemu ya mazoezi, tukishaanza ligi tutacheza vizuri.
Tumefanya mazoezi ya kutosha na nimeridhika na uwezo wa kila mchezaji,"alisisitiza Milovan ambaye timu yake itaondoka jijini hapa leo Jumanne kurejea Dar es Salaam.
Simba imecheza mechi tatu za kirafiki jijini hapa dhidi ya Mathare United, Oljoro JKT na Sony Sugar. Dhidi ya Mathare na Oljoro
walishinda mabao 2-1 huku ikitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Sony.
SOURCE; GAZETI LA MWANASPOTI
No comments:
Post a Comment