
MICHUANO ya Super8 iliendelea jana kwa mechi nne kwenye viwanja tofauti, huku Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 mjini Moshi, na Azam FC ikipokea kipigo kama hicho mbele ya kocha wao mpya, Boris Bunjak Uwanja wa Chamazi.
Kwenye Uwanja wa Ushiriki, kikosi cha Simba kinachoundwa na wachezaji wengi kutoka timu B, kilipoza majeraha ya kipigo cha mabao 3-1 na City Stars ya Kenya katika siku yao maalum (Simba Day) Jumatano iliyopita kwa kuifunga Mtende ya Zanzibar.
Shujaa wa ushindi wa Simba katika mchezo huo alikuwa mshambuliaji Edward Christopher aliyetikisa mara zote mbili kamba za timu ya Mtende.
Alifunga bao la kwanza kwa shuti kali dakika 11 tangu kuanza mchezo, na akaongeza lingine dakika ya 26 kwa mkwaju wa penalti.
Mtende wangeweza kupunguza mabao hayo na kufanya matokeo kuwa 2-1, lakini mchezaji wake Yahya Tumbo alishindwa kufunga penalti waliyopata katika dakika ya 38.
Katika mchezo wa Chamazi, Mtibwa ilicheza vizuri na kuwafunika wenyeji wao Azam na kujipatia mabao yao yote kipindi cha pili.
Kocha Banjak hakuwa kwenye benchi la Azam, lakini alishuhudia kutoka jukwaani vijana wake anaotarajia kuwafundisha wakishindwa kwenda sambamba na moto wa Mtibwa.
Mshambuliaji Gaudence Mwaikimba, nusura aipeleke mbele Azam kama siyo kupata kigugumizi cha kuukamisha wavuni na kupiga nje mpira akiwa yeye ni kipa wa Mtibwa.
Naye Hassan Seif wa Mtibwa atajutia nafasi nzuri ya kufunga aliyoipata dakika ya 40, baada 'kuulemba' mpira na kutaka kufunga kwa kisigino, lakini akaishia kuupiga nje.
Shaban Kisiga wa Mtibwa, alionyesha jitihada binafsi baada ya kuwachezea 'drafti' mabeki wa Azam na kupiga kiki kali iliyomshinda Mwadini Ally na kujaa wavuni dakika ya 54.
Jahazi la Azam iliyocheza fainali ya Kombe la Kagame na kufungwa na Yanga 2-0, lilididimia tena dakika ya 77 baada ya Mtibwa kufunga bao la pili kupitia Hussein Javu.
Kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, timu ya Polisi Moro iliibuka na ushindi wa maba 2-0 dhidi ya timu ya Super Falcon ya Zanzibar.
Mabao ya washindi katika mchezo huo yalifungwa na Nico Kabite katika dakika ya 50, kabla ya Malini Busungu kuongeza lingine dakika ya 74.
Imeandikwa na Moses Mashala (Arusha), Miguel Suleiman (Mwanza) Clara Alphonce
No comments:
Post a Comment