tuwasiliane

Wednesday, July 25, 2012

25 JUL.Simba yamkatia rufaa Yondani kwa Tibaigana


UONGOZI wa Simba umesema licha ya uamuzi wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji kuamua Kelvin Yondani (pichani) aichezee Yanga katika michuano ya Kagame, kwa upande wao tayari wameshakata rufaa katika Kamati ya Nidhamu ya TFF inayoongozwa na kamishna mstaafu wa polisi, Alfred Tibaigana.
Yondani amesaini mkataba wa kuichezea Yanga, lakini Simba imekuwa ikidai kuwa mchezaji huyo ni halali kwao kwani kabla hajajiunga na Yanga alikuwa na mkataba wao, ila ulikuwa na tatizo la uchapaji badala ya kuonyesha unaanza Desemba 2011 ulionyesha unaanza Desemba 2012.

Akizungumza na Championi Jumatano juzi, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Alex Mgongolwa, kuamua Yondani aichezee Yanga katika michuano ya Kagame imekuja wakati wao tayari wakiwa wameshakata rufaa katika kamati ya Tibaigana, hivyo wanasubiri uamuzi wa kamati hiyo ambayo ni ya juu zaidi.

“Sisi tayari tumeshakata rufaa katika kamati ya nidhamu chini ya Alfred Tibaigana na sasa tunasubiri uamuzi wa mwisho ili tuweze kuona hatima ya mchezaji huyo.
“Uamuzi wa Mgongolwa ulikuja huku tukiwa tayari tumeshakata rufaa katika kamati ya Tibaigana, hivyo tunaamini tutashinda kwani Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ni ndogo zaidi ya kamati ya Tibaigana,” alisema Kamwaga.

Alisema wanaamini kila kitu kitakwenda sawa juu ya mchezaji huyo kwa kuwa mkataba walionao ni halali.
SOURCE; GLOBAL PUBLISHERZ

No comments:

Post a Comment