
William Malecela, mtoto wa mwanasiasa mkongwe nchini, John Malecela, amemshukia Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama, akisema amepitwa na wakati na hana uwezo wa kuongoza chama hicho katika mazingira ya sasa.
Katika mchango wake katika mtandao wa jamii wa Jamii Forum, William alisema Mukama hawezi kukimbizana na siasa za sasa.
“Sina uhakika kama bado Mkama anaweza kukimbizana na siasa za sasa, kama ni kweli ameandika barua ya kujiuzulu then ingekuwa ni kwa sababu ya kukubali kupitwa na wakati wa modern politics, lakini siyo kwa sababu ya Nape.
“Haya ndiyo mambo niliyoyasema Mlimani TV, CCM ifike mahali ibadilike, iwe sawa na wananchi inaowaongoza maana so far haiko hivyo,” alisema.
William, ambaye ni mjumbe wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Dar es Salaam na CCM Wilaya ya Ilala, alisema kimsingi kazi anayoifanya Nape ni nzuri, ambayo ni kwa ajili ya chama na mwenyekiti pia.
“Nape ni kijana makini ambaye ni muhimu katika mkakati wa siasa, kwa sababu anafikiri haraka katika nafasi yake, na anaelewana na Januari Makamba. Wote wawili wanaweza kufikiri na kutoa majibu kwa haraka ambayo ni sauti, kitu ambacho ni kigumu sana kukipata ndani ya CCM, wengi wamekuwa na mazoea ya kusubiri mwenyekiti,” alisema.
Mtoto huyo wa Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM Tanzania Bara, alisema chama hicho kinasumbuliwa na msongo wa uchaguzi wa mwaka 2005, lakini mpaka leo haujaisha na kukifanya kuwa makini katika mkakakati.
“Zile stress (msongo) bado hazijaisha na haukufanyika mkakakati makini baina ya wanachama kumaliza zile tofauti za kambi za uchaguzi, na pia ‘washikaji’ waliomsaidia Rais wa sasa kuingia madarakani na kushindwa matarajio yao ya kufanya lolote wanalotaka kwa sababu tu ni washikaji,” alisema.
“Siamini hata kwa dakika kwamba Nape anajichukulia madaraka, lakini ninaamini kwamba anafanya kazi kwa muda na mazingira tulionao sasa, ambayo ni magumu sana kulinganisha na viongozi kama Mukama.
“Namaanisha hawa wote ni rafiki zangu wazuri, lakini kwa taarifa za hili gazeti siogopi kusema kwa sababu kama kweli unakipenda chama na kwa faida ya baadaye huwezi kusema kwamba Nape anakivuruga chama, labda kama una suala binafsi,” alisema William.
Katika mtandao huo, William alisema tatizo la wanasiasa wakubwa wa Tanzania ni kwamba hawana washauri wanaofaa, wengi wamejijazia washauri waliopitwa na wakati.
Alisema anaunga mkono harakati za Nape kwa asilimia 100 kwa sababu anakisaidia chama na yeyote anayedai kwamba anakivuruga ina maana moja tu, hana nia njema na chama hicho.
“Nape anafanya kazi inavyotakiwa kama kufikiria kwa haraka na kutoa uamuzi mgumu bila kumsubiri mwenyekiti kwa kila kitu, ni lazima itakuwa inawaudhi baadhi ya waliozoea kukimbilia kwa Mwenyekiti kila wakati.
“Juzi nilikuwa kiwanjani kwenye mechi ya wabunge, nilikuwa karibu na kiongozi mmoja mkubwa wa CCM nikamwambia subiri Zitto na Nassari watakapotajwa kuingia uwanjani utaona kelele za wananchi, akaniuliza kwa nini, nikamjibu ni kwa sababu wanafanana na wananchi wengi waliopo hapa uwanjani.
“Wakati umefika wa CCM kuanza kubadilika ifanane na wananchi inaowaongoza, sina tabia ya kuzunguka mbuyu, viongozi kama Mkama wabaki nyuma kutoa ushauri lakini hatuwezi tena kuwa nao mbele katika sura ya chama wakati umepita,” alisema William.
No comments:
Post a Comment