Kalunde Jamal
MCHEZAJI wa timu ya taifa na Azam, John Boko amesema wanakwenda Msumbiji wakiwa na dhamira ya kweli ya ushindi huku akiwashukuru Watanzania kwa jinsi walivyowaungwa mkono katika mechi dhidi ya Gambia.
Boko alisema mashabiki wa soka mwishoni wiki wakati Taifa Stars ilipokuwa ikicheza na Gambia walijitokeza kwa wingi na kuonyesha umoja wa hali ya juu kwa kuishangilia Stars bila kuchoka.
Alisema umoja ulioonyeshwa na mashabiki wa soka kwenye mchezo dhidi ya Gambia uliwapa hamasa kubwa ya kufanya vizuri pia umoja ule umekuwa chachu ya kutafuta ushindi kwenye mchezo ujao dhidi ya Msumbiji.
"Nafurahi kucheza kwenye timu hii ambayo kiwango chake kinabadilika siku hadi siku hata ukiangalia wachezaji wote tumekuwa wepesi, lakini shukrani za pekee ziwaendee viongozi wangu wa klabu ya Azam kwa kunipa moyo wa kurudi kuichezea timu hii,"alisema Boko.
"Nafurahi zaidi kuona wachezaji na viongozi tumekuwa kitu kimoja na ndiyo kitu kinachomfurahisha mwalimu yaani kushirikiana ndani ya uwanja na nje ya Uwanja,"alisema Boko.
Boko aliwataka Watanzania kuwa na subira na kukubali matokeo yanapokuwa sio mazuri kwa kuwa hakuna aliyekamilika na nia ya timu ni kupata ushindi na sio kushindwa.
"Umoja ndio kila kitu nawapa pongezi Watanzania hasa wapenda soka kwa kurudi kule tulikotoka miaka michache iliyopita yaani ya kila mmoja kujiona anahusika na timu ya taifa na kuachana na Usimba na Uyanga ambao kwa kiasi fulani huwakatisha tamaa wachezaji, kitendo cha kuungana na kuwa pamoja kwenye mchezo ule nakipongeza sana,"alisema Boko kwa furaha.
Boko na wachezaji wenzake wa Taifa Stars wanatarajiwa kuondoka nchini Ijumaa kuelekea Maputo kwa ajili ya kucheza mechi ya maridiano dhidi ya Msumbiji ya kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa Afrika zitakazofanyika Afrika Kusini 2013.
Katika mechi ya kwanza iliyozikutanisha Msumbiji na Taifa Stars jijini Dar es Salaam matokeo yalikuwa ni sare ya 1-1.
No comments:
Post a Comment