POLAND 1 RUSSIA 1
Wenyeji Poland walionyesha mchezo wa hali ya juu katika uwanja wa Warsaw dhidi ya Urusi, mechi iliyokwisha kwa sare ya 1-1.
Poland na Urusi
Poland imejiongezea matumaini ya kuvuka salama mechi za makundi
Hii ilikuwa ni mechi ya pili siku ya Jumanne.
Kwa sare hiyo, Poland ina matumaini kwamba huenda ikavuka mechi za makundi.
Poland, ambayo inashirikiana na Ukraine katika kuandaa mashindano ya Euro 2012, tayari ilikuwa imelemewa bao 1-0 kabla ya kufanikiwa kusawazisha, kupitia nahodha Jakub Blaszczykowski katika kipindi cha pili, na kwa mkwaju wa mguu wa kushoto.
Urusi walikuwa wamefanikiwa kuongoza walipopata bao katika dakika ya 37, kupitia mshambulizi hodari Alan Dzagoev baada ya kupigiwa pasi safi na Andrey Arshavin.
Timu zote zilionyesha mchezo wa hali ya juu, na kulikuwa na uwezekano wa kila timu kujipatia ushindi.
Matokeo hayo yanamaanisha ushindani ni wazi katika kundi A, na kimahesabu timu zote nne katika kundi hilo zinaweza kufuzu kuingia robo fainali.
Kabla ya mechi hiyo, mashabiki wa Urusi walikuwa tayari wamewaudhi wenyeji Poland katika mji mkuu wa Warsaw.
Mashabiki wa Urusi, katika kuadhimisha siku kuu ya uhuru wao, waliendeleza sherehe zao katika barabara za Warsaw, jambo ambalo liliwaudhi wenyeji, na kuwafanya polisi wa kutuliza ghasia kuingilia kati na kujitahidi kuwatawanya mashabiki wa pande zote mbili
CZECH 2 GREECE 1
Juhudi za Jamhuri ya Czech kufanya vyema katika mashindano ya Euro 2012 zilipata nguvu Jumanne, kwa kuishinda Ugiriki magoli 2-1, mabao ya haraka katika dakika sita za mwanzo.
Ugiriki walikuwa mabingwa mwaka 2004, lakini uhodari wao bado haujajitokeza katika mashindano ya mwaka huu.
Petr Jiracek alifunga bao la kwanza katika mechi hiyo, dakika ya tatu.
Vaclav Pilar aliongezea bao la pili.
Ugiriki wakidhani wamepata bao, mwamuzi alilifutilia mbali kwa kusema walikuwa wameotea.
Hata hivyo, katika kipindi cha pili, kufuatia kosa la kipa wa Czech, Peter Cech, Ugiriki waliweza kujituliza kwa goli moja kupitia Fanis Gekas.
Cech, mwenye umri wa miaka 30, na ambaye ni kipa makini katika klabu ya Chelsea, katika mashindano haya amefungwa magoli matano tayari, lakini bila shaka atashukuru aliweza kuepuka makosa zaidi, na nchi yake ikaondoka na ushindi.
No comments:
Post a Comment