
EDO KUMWEMBE, ABIDJAN
MSHAMBULIAJI wa Chelsea anayeondoka klabuni hapo, Didier Drogba amempigia saluti na kumtania mshambuliaji wa Taifa Stars, Mbwana Samatta akimwambia: Naondoka Chelsea njoo uchukue jezi yangu.
Drogba aliyasema hayo baada ya kuulizwa ni mchezaji gani aliyemvutia kwa upande wa Taifa Stars muda mchache baada ya mechi hiyo kumalizika wakati anakaribia kuondoka uwanjani hapo mwishoni mwa wiki.
Yule ambaye alikuwa anasumbua timu yetu, mgongoni amevaa jezi namba 10, ni mzuri yule, anacheza wapi? Mwambie naondoka Chelsea aje kuchukua jezi yangu, alisema Drogba.
Drogba pia alikiri kwamba Taifa Stars ilikuwa katika kiwango kizuri katika pambano hilo na kwamba walicheza vizuri kuliko pambano la kirafiki walilocheza dhidi yao Februari mwaka 2010 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ilikuwa katika kiwango kizuri sana tofauti na tulivyocheza mara ya mwisho. Hata hivyo wachezaji inabidi waongeze nguvu kwa sababu wakati mwingine ni shida sana unapocheza na wachezaji wenye nguvu kama sisi, aliongeza Drogba.
Katika pambano hilo, Drogba alifunga bao la pili kufuatia krosi nzuri ya winga mahiri Kader Keita ambaye aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Gervinho na kuisumbua vilivyo safu ya Taifa Stars.
Stars ililala kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Solomon Kalou na Drogba.
No comments:
Post a Comment