tuwasiliane

Monday, April 30, 2012

30 APR.Azam waiadhibu 3 Toto Africa 1


AZAM FC jioni hii imezima ndoto za Simba SC kutwaa mapema ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa Toto African ya Mwanza mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Azam, Chamazi, Dar es Salaam.

Azam imetimiza pointi 56 na ikishinda mechi yake ya mwisho dhidi ya Kagera Sugar itatimiza pointi 59, sawa na za Simba iliyobakisha mechi moja tu na Yanga Mei 5. Iwapo Simba itafungwa na Yanga na Azam ikaifunga Kagera, ina maana kwa mara ya pili mfululizo msimu huu, bingwa wa Ligi Kuu ataamuliwa kwa wastani wa mabao.

Katika mchezo wa leo, Azam FC walianza kulisakama lango la Toto huku mshambuliaji wa timu hiyo John Bocco akikosa bao baada ya kupiga shuti lililotoka nje.

Toto African walijibu mashambulizi hayo kwa kulisakama lango la Azam lakini, Enyinna Barlinton alikosa bao.

Azam walianza kuhesabu bao la kwanza katika dakika ya 10 kupitia kwa Kipre Tcheche huku Tcheche akifunga bao la pili katika dakika ya 19.

Azam walizidi kuliandama lango la Toto na katika dakika ya 34, Bocco aliipatia timu yake bao la tatu baada ya kupokea pasi ya Tcheche. Na goli hilo linamfanya aweke rikodi mpya ya klabu ya kufunga magoli mengi katika msimu mmoja, ambapo alifunga goli lake la 17 katika msimu huu wa ligi kuu ya vodacom.

Toto walifanikiwa kupata bao la kufutia machozi katika dakika ya 85 kupitia kwa Enyiama Darlington.

Azam FC: Mwadin Ali, Erasto Nyoni, Waziri Omary, Luckson Kakoloki, Agrey Morris, Ibrahim Mwaipopo, Mrisho Ngasa, Kipre Tcheche, Bolou Kipre, John Bocco, Salum Salum.

Toto Africa: Mustafa Mabrouk, Idd Mobby, Eric Muliro, Peter Mutabuzi, Ladislaus Mbogo, Laban Kambole, Emanuel Swita, Mohamed Soud, Enyiama Darlington, Kamana Salumu, Mussa Said.

No comments:

Post a Comment